Monday, February 20, 2012
20 FEB.Papic awapoza mashabiki Yanga
KOCHA Mkuu wa Yanga Kostadin Papic amewakingia kifua washambuliaji wake Kenneth Asamoah na Davies Mwape kutokana na kupoteza nafasi nyingi za wazi za kufunga kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa ya Afrika dhidi ya Zamalek kwenye Uwanja wa Taifa juzi.
Kwenye mchezo uliomalizika kwa Yanga kulazimishwa sare ya bao 1-1 na miamba hiyo ya zamani ya soka ya Afrika washambuliaji hao kutoka Ghana na Zambia walipoteza nafasi nyingi za kufunga kitendo kilichoonekana kuwakera manazi wa timu hiyo kongwe nchini.
Akizungumza mara baada ya mechi hiyo Papic alisema kuwa amewachezesha washambuliaji hao kwenye mechi hiyo kwa sababu amekuwa akiwatumia pamoja kwenye mechi mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Alisema jambo la kukosa nafasi za kufunga ni la kawaida kwenye mchezo wa soka na kwamba kama ingetokea wachezaji hao wamefunga kwenye mechi hiyo hakuna mtu ambaye angehoji kwa nini amewapanga.
Papic alisema kuwa yeye ndio kocha wa timu hiyo anapanga wachezaji wa kucheza kulingana na uwezo wao na kwamba hana sababu ya kutoa maelezo kwa kila maamuzi anayofanya juu ya upangaji wa timu hiyo.
“Kama kocha wa timu sina sababu ya kueleza kila uamuzi ninaochukua juu ya upangaji wa timu yangu, huo ndio mpira mara nyingine unacheza vizuri, mara nyingine unakuwa chini ya kiwango,”alisema kocha huyo kutoka Serbia.
Hata hivyo hasa baada ya mashabiki wa timu hiyo kuanza kupiga kelele ya kumtaka kocha huyo kufanya mabadiliko ndipo alipoamua kumtoa Davies Mwape na kumuingiza Shamte Ali, mabadiliko ambayo hayajainufaisha Yanga kwani Zamalek walisawazisha kupitia kwa mshambuliaji wake Amri Zaki. Zaki aliingia kipindi cha pili badala ya Ahmedi Fathi Abdelsamea.
Aidha, Papic alisifu kiwango kilichooneshwa na timu yake kwenye mchezo huo na kudai ni miongoni mwa mechi chache ambazo timu hiyo imecheza msimu huu na kudai bado wanayo nafasi ya kufanya vizuri kwenye mchezo wa marudiano utakaochezwa Cairo wiki mbili baadaye.
Alisema bado hajakata tamaa na kwamba ngwe ya kwanza imemalizika na sasa wanajipanga kwa ngwe ya pili ambapo timu hizo zinatarajia kukutana baada ya wiki mbili huko Cairo, Misri, ambapo Yanga itapaswa kupata ushindi wa aina yoyote ili isonge mbele.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment