tuwasiliane

Monday, February 20, 2012

20 FEB. COASTAL YAZIDI KUTAKATA


COASTAL Union jana iliweka rekodi Ligi Kuu bara baada ya kuifunga Ruvu Shooting bao 1-0, ukiwa ni ushindi wa tano mfululizo katika mechi mechi sita ilizocheza tangu kuanza mzunguko wa pili.

Shujaa aliyeihakikishia ushindi Union, alikuwa Said Sued aliyefunga bao hilo kwa kiki ya adhabu ndogo iliyopenya katikati ya miguu ya kipa wa Ruvu, Benjamin Henga katika dakika ya 55.

Tangu mzunguko huu wa pili uanze Coastal Union imefungwa na Simba 2-1 , lakini baada ya hapo imeichapa Mtibwa bao 1-0, Moro United 1-0, African Lyon 1-0, JKT Ruvu 2-0 na hivi sasa imeichapa Ruvu Shooting 1-0.

Kwenye uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro timu ya Mtibwa Sugar imeendeleza wimbi la ushindi baada ya kuifunga Villa Squad mabao 2-1.

Mabao ya Mtibwa yalifungwa na Vicent Barnabas katika dakika ya 15 baada ya kuwatoka mabeki wa Villa na bao la pili la Mtibwa lilifungwa na Said Bahanuzi katika ya dakika 75 kwa mkwaju wa penati.

Nsa Job ameendelea kuwadhihirishia mashabiki wa soka nchini kuwa yeye ni shujaa, baada ya kuifungia klabu yake bao pekee katika dakika ya 35.

Mjini Dar es kwenye uwanja wa Chamazi timu za African Lyon na Oljoro JKT zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya 2-2.

Timu zote zilianza kwa kushambualina ila katika dakika ya 19 Rashid Roshwa aliipatia Oljoro bao baada ya kupiga shuti lililomzidi mguvu kipa wa Lyon, Abdul Seif na kujaa wavuni.

Vijana wa African Lyon walisawazisha bao hilo katika dakika ya 29 kupitia kwa Kassim Selembe aliyefunga kwa kichwa cha kuparaza krosi iliyopigwa na Hood Mayanja.

Lyon baada ya kupata bao hilo la kusawazisha walipata nguvu na kufanya mashambulizi mengi langoni mwa Oljoro hata hivyo timu hizo zilienda mapumziko zikiwa zimefungana bao 1-1.

Kipindi cha pili timu zote zilikuwa zikishambuliana kwa zamu, lakini walikuwa Oljoro, ambao walipata bao la pili baada ya nahodha wa wao Paul Nonga kupiga shuti la umbali wa mita 35 na kwenda moja kwa moja nyavuni.

Katika dakika ya 71 vijana wa Lyon walisawazisha bao hilo ambalo lilifungwa na Samwel Ngasa akiunganisha krosi ya Justine Anene.

Kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Timu ya Polisi Tanzania na Moro United zilishindwa kutambiana pia baada ya kutoka sare ya 1-1.

Mabao yote ya timu hizo yalipatikana katika kipindi cha pili, ambapo Moro United walikuwa wa kwanza kupata bao kwa mkwaju wa penati uliopigwa na Godfrey Wambura katika dakika ya 73 baada ya Delta Thomas kuunawa mpira ndani ya 18.

Lakini pia Polisi Dodoma walisawazisha bao hilo kwa mkwaju wa penati uliopigwa na Ibrahim Masawe baada ya beki wa Moro, Fred Mbuna kuunawa mpira pia akiwa katika eneo la hatari.

No comments:

Post a Comment