tuwasiliane

Saturday, February 18, 2012

18 FEB SIMBA NA YANGA VITANI LEO


MABINGWA wa soka nchini, Yanga leo watashuka dimbani wakiwa na deni la kucheza kufa na kupona ili kuepuka kuithibitisha kauli ya wapinzani wao Zamalek ya Misri kwamba, wamekuja nchini kuwafanya wao kuwa ngazi ya kutwaa ubingwa wa Vilabu Afrika.

Mchezo huo ulioteka hisia za mashabiki wa soka nchini, unatarajia kuwa mkali ndani ya Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia majira ya saa 10 jioni.

Jana katika mkutano na waandishi wa habari jijini, Kocha Msaidizi wa Zamalek, Ossama Nabil alisema wamekuja Tanzania siyo tu kuifunga Yanga, bali nia yao kubwa ni kutwaa ubingwa baada ya muda mrefu.

Nabil alisema ni muda mrefu sasa umepita bila timu yao kutwaa taji kubwa la soka Afrika, hivyo fursa ya pambano la leo dhidi ya Yanga ambalo wana hakika watashinda ni njia nzuri kuelekea kurejesha taji hilo.

"Tunaiheshimu Yanga kama klabu kubwa na yenye uzoefu kwenye michuano hii, lakini pamoja na hilo kwa upande wetu tunataka kulirudisha kombe la michuano hii katika mikono yetu baada ya kulikosa kwa muda mrefu," alisema kocha huyo msaidizi.

"Tumekuja hapa siyo tu kuifunga Yanga, lakini pia mechi ya hiyo ni fursa yetu nzuri ya safari ya kutwaa taji tulilolikosa kwa muda mrefu sasa," alisema Nabil kwa kujiamnia.
Nabil alisema kuwa kikosi chake kiko imara na chenye kila utayari wa ushindani dhidi ya Yanga. "Tumekuja tukiwa tumejiandaa vizuri, tumekuja kufurahia ushindi."

Kwa upande wa Kocha, Kostadin Papic ambaye mwanzoni alionyesha kukata tamaa ya kuzaimisha Zamalek nyumbani, jana alitoa kauli za kujivunia maandalizi aliyofanya kwenye kikosi chake.

"Nimemaliza jukumu la maandalizi kwa timu yangu, nimendaa kikosi cha ushindani kinachojiandaa kukabiliana vizuri na Zamalek," alisema Papic katika mkutano na waandishi wa habari.

Papic hakutaka kuibeza Zamalek kama alivyofanya mwenzake, lakini yeye anaamini anacheza na moja ya timu bora kabisa katika soka la Afrika.

"Kama kocha nimemaliza kazi yangu, ninaweza kusema tupo tayari kupambana na Zamalek katika pambano hili gumu. Hatuna la zaidi uwanjani zaidi ya ushindi," alisema Papic

Pamoja na maandalizi hayo, Papic atashusha kikosi kitakachokuwa na makali pungufu kutokana na baadhi nyota wake kuwa nje kutokana na kuwa majeruhi.

Ni wazi kipa namba moja, Yaw Berko hatakuwa uwanjani leo, sawa kama ilivyo kwa viungo Salum Telela, Godfrey Bonny, Nurdin Bakar na Rashid Gumbo.

Na badala yake, Yanga itawategemea zaidi washambuliaji wake Devis Mwape na Kenneth Asamoa kupeleka mashambulizi langoni mwa Zamalek wakipitishiwa mipira na kiungo Haruna Niyonzima.

Kwa upande wa kikosi cha mafarao, mshambuliaji zamani wa Wigan Athetic, Amri Zaki ndiye anayetarajia kuwa mwiba mkali kwa Yanga sambamba na Mcameroon Alex Mdomo na Razack Thomas ambaye ni raia wa Benin.
Wakati huo huo, nyota wa zamani wa Yanga, Athuman Chama 'Jogoo' amemtaka kocha wa timu hiyo, Mserbia Kostadin Papic kutumia mfumo wa 4-4-2 badala ya 4-3-3 kwenye pambano la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek.

Beki huyo wa zamani wa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars alisema: "Tangu Papic alivyotua nchini mwaka jana kukinoa kikosi cha Yanga amekuwa akitumia mfumo wa 4-3-3," alisema Chama.
Amekuwa akiwachezesha Mwape, Asamoah na Kiiza nafasi ya ushambuliaji wakati Kijiko, Seme na Niyonzima wakicheza katikati ya kiwanja.

"Sioni kama mfumo huo unatoa matumaini chanya yakuishinda Zamalek kwa leo, ambao wana uwezo mkubwa wakumiliki mpira na kupiga pasi kutoka njuma hadi mbele kushambuliaji," alisema Chama.

Alisema anafikiri mfumo wa 4-4-2 ndio utatoa nafasi kubwa kwa Yanga kuweza kuwadhibiti vilivyo Waarabu hao.
"Unavyotumia mfumo wa 4-4-2 ina maana utakuwa na wachezaji wanne katikati ya kiwanja ambao watakuwa na kazi ya kuzuia na pia kushambulia kwa wakati mmoja," aliongeza Chama.

"Lakini unavyotumia 4-3-3 unapunguza mtu mmoja katikati ya uwanja na kumpeleka mbele kushambulia, zitaki kuamini kwamba Kiiza ana uwezo wa kucheza kama kiungo mshambuliaji," alisema.

Alishauri kocha huyo kutumia mfumo wa 4-4-2 kwa lengo la kuwadhitibiti Zamalek na kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye pambano hilo la awali na kujiweka katika mazingira mazuri kusonga mbele ya michuano hiyo. WAKATIHUOHUO WASHINDI wa pili wa Kombe la CAF mwaka 1993, Simba wanashuka kwenye Uwanja wa Nyamirambo jijini Kigali kuwakabili wenyeji Kiyovu katika mchezo wa kwanza wa kusaka kufuzu kushiriki hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho.

Simba watashuka dimbani saa 9.30 za Rwanda, ambapo ni sawa na saa 10.30 za hapa Tanzania wakiwa na kumbukumbu ya ushindi mnono wa mabao 2-0 dhidi ya Azam ulioifanya ibaki kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania.

Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi ambaye ameishafunga mabao 9 katika Ligi Kuu, leo atacheza akiwa na swahiba wake na Mzambia, Felix Sunzu kwenye safu ya ushambuliaji.

Sunzu aliyemshuhudia mdogo wake Stopila Sunzu akiingoza Zambia kutwaa Kombe la Mataifa Afrika mwaka huu, atakuwa na jukumu la kuhakikisha anatengeneza nafasi za kutosha kwa Okwi ili kuiweka Simba katika nafasi nzuri ya kuwania kuingia raundi ya pili.

Vinara hao wa Ligi Kuu ya Tanzania mwaka jana walipoteza mafasi ya kufuzu kuingia hatua ya makundi baada ya kutolewa na DC Motema Pembe ya DR Congo, ambapo msimu huu wamerudi upya wakiwa chini ya kocha Milovan Cirkovic anayependa kutumia staili ya kushambulia kwa kushtukiza na kujilinda kwa umakini.

"Tutaingia uwanjani kutafuta ushindi siyo kukaa nyuma na kuwasubiri wapinzani wetu, tumekuja hapa kupambana na kuhakikisha tunapata goli la ugenini sio kingine," alisema Milovan Cirkovic.

Pamoja na ndoto hiyo ya Milovan, kocha huyo anatakiwa kuhakikisha ngome yake ambayo itakuwa chini ya Juma Nyoso na Kelvin Yondani inaepuka kufanya makosa ya kizembe ili Kiyovu wasitengeneze nafasi za kumfikia Juma Kaseja kirahisi.

Kiungo Patrick Mafisango atakuwa na kazi kubwa ya kuwaongoza Mwinyi Kazimoto na Shomari Kapombe katika kuhakikisha wanatibua mipango yote ya Kiyovu.

Nahodha wa Simba, Juma Kaseja alisema hawataki kuangalia matokeo yao ya nyuma ila watakachokifanya ni kuhakikisha wanashinda mechi ya leo.

"Unaposhinda kila kitu kibaya kinasahaulika na hicho ndicho tunachotaka kufanya hapa,"alisema Kaseja.
Mabeki wa Simba watalazimika kuwa makini zaidi na Mayanja kwani tangu aliposajiliwa na Kiyovu FC akitokea SC Villa ameisaidia klabu hiyo kupanda hadi nafasi ya nne katika Msimamo wa Ligi ya Rwanda.

Mayanja ni kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za kufunga kwa pamoja na uwezo wa kupiga mashuti yanayolenga goli kwa kutumia miguu yote.

Kocha wa Kiyovu, Jean Baptiste Kayiranga akiizungumzia mechi dhidi ya Simba alisema, “tumekiimarisha kikosi chetu kwa kusajili nyota watatu wa Uganda na wawili wa hapa ndani tayari kwa kuivaa Simba.”

Mwamuzi wa akiba atakuwa Hudu Munyemana kutoka Rwanda, huku kamishna wa mechi hiyo akiwa ni Abbas Sendyowa kutoka Uganda. Mechi ya marudiano imepangwa kufanyika Machi 4.

Mshindi kati ya Simba na Kiyovu atakutana na Entente Sportive (ES) Setif ya Algeria kwenye hatua ya 16 bora baadaye mwaka huu.

UWANJA
Mechi ya leo itapigwa kwenye uwanja wa Nyamirambo unaotumia nyasi za bandia kama wa Uhuru au Azam Complex kutokana na ule wa Amahoro kuwa kwenye matengenezo hivi sasa.

HALI YA HEWA
Jiji la Kigali lipo juu, hivyo hali ya hewa yake ni baridi wakati wa asubuhi na usiku, lakini mchana ni jua kali na joto kama ilivyo katika jiji la Arusha.

No comments:

Post a Comment