
SHIRIKISHO la Soka Nchini (TFF) limesema linasubiri taarifa kutoka Shirikisho la Soka la
Afrika (CAF) na Chama Cha Soka nchini Misri (EFA) kuhusu hali ya usalama nchini Misri.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah akizungumza jana, alisema wanaamini CAF na EFA watakuwa wanafuatilia kwa makini hali ya usalama ndani ya Misri na kama wataona hali bado ni tete ni wazi watawajulisha nini cha kufanya.
Yanga ya Dar es Salaam itacheza na Zamalek ya Misri katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwanzoni mwa mwezi ujao jijini Cairo, misri ambao mechi ya kwanza baina ya timu hizo itafanyika jijini Dar es Salaam Machi 18 mwaka huu.
Hatua ya Osiah inafuatia swali aliloulizwa na 'Habarileo' kuhusiana na usalama wa Yanga itakapoenda Misri kutokana na matukio ya vurugu za mashabiki wa Zamalek yaliyotokea Jumatano kwa kuchoma Uwanja wa Cairo na pia vurugu nyingine za mashabiki kwenye mechi kati ya Al Masry na Al Ahly iliyosababisha mashabiki 74 kufa uwanjani.
Osiah alisema anachofahamu kuwa vurugu zilizotokea nchini Misri sasa hivi ni za mashabiki lakini kama zitakuwa ni za nchi nzima hilo litakuwa suala lingine na kwamba wana imani CAF na EFA watafanyia kazi matukio hayo.
Naye Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema kuwa suala la usalama wa timu hiyo itakapoenda nchini Misri ni jukumu la CAF na EFA. Alisema kama EFA na CAF wataona hali ya usalama katika Jiji la Cairo sio shwari basi mechi hiyo watahamishia kwenye miji mingine mfano Alexandria au ikibidi kuchezwa nje ya nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment