tuwasiliane

Tuesday, January 31, 2012

31 JAN.AZAM YAZISOGELEA SIMBA NA YANGA


AZAM FC jana ilitumia vizuri uwanja wa nyumbani Chamazi kuendeleza mbio za kuzifukuza Simba na Yanga kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, baada ya kuifunga Moro United bao 1-0, shukrani kwa mshambuliaji John Bocco aliyefunga bao peke katika mchezo huo.

Kwa ushindi huo, Azam--mabingwa wa Kombe la Mapinduzi wamefikisha pointi 29 baada ya kucheza mechi 14, ikiwa nyuma kwa pointi mbili tu dhidi ya vigogo Simba na Yanga.

Katika mchezo huo, Azam wangeweza kuibuka na ushindi mnono kama washambuliaji wake wake wangetumia nafasi nyingi za kufunga walizopata hasa katika kipindi cha kwanza.

Bocco alifunga bao hilo katika dakika ya 11 kwa shuti kali baada ya kuwalamba chenga mabeki wa Moro United kufuatia ushirikiano mzuri na mshambuliaji mwenzake, Kipre tchche.

Azam wangeweza kufanya matokeo kuwa 2-0 mpaka dakika ya 25 kama siyo Kipre kupoteza nafasi nzuri ya kufunga, huku pia shuti lake la dakika ya 40 likigonga mwamba wa goli.

Shambulizi kubwa walilofanya Moro United kipindi cha kwanza, lilikuwa katika dakika ya 25 baada ya Kalvin Chale kupiga mpira wa adhabu ndogo uliotemwa na kipa wa Azam Mwadin Ally.

Kipindi cha pili, Moro United walioneka kucheza kwa kuelewana na nusura Geofrey Wambura afunge bao katika dakika ya 52 lakini akaishia kupaisha mpira juu pasi ya Fred Mbuna.

Winga Mrisho Ngassa alikosa bao la wazi katika dakika ya 68, baada ya kutereza ndani ya eneo la hatari wakati akijiandaa kupiga mpira kufuatia kuwatoka mabeki wa Moro United.

Kocha wa Moro United, Hassan Banyai alisema ameridhika na kipigo hicho, lakini alimtupia lawama mwamuzi aliyechezesha pambano hilo kwa madai ya kutokuwa makini kufuatilia sheria za za mchezo wa soka.
Banyai amesema ameridhishwa na kiwango walichoonyesha vijana wake na sasa anajipanga kwa ajili ya mechi ijayo.

Hall Stewart, kocha wa Azam alisema amefurahishwa na matokeo hayo kwani muhimu ni pointi tatu ambazo vijana wake wamezipata. Hata hivyo, alisema baada ya bao la kwanza wachezaji wake walijisahau na kuwafanya Moro United kurejea kwenye mchezo tofauti na kipindi cha kwanza.

No comments:

Post a Comment