
Aliyekuwa Mwenyekiti wa timu ya kampeni ya Rais Kikwete mwaka 2010, Abdurhaman Kinana ni miongoni mwa makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanaolalamikia mbio za urais zinavyoathiri utendaji wa chama tawala na serikali.
Kwani Mgomo huo wa madaktari, mbio za urais wa mwaka 2015 na kupanda kwa gharama za maisha ni miongoni mwa mambo yanayoutikisa na kutishia mustakabali wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete.
Viongozi na makada mbalimbali wa chama hicho tayari wameshaanza kulalamikia harakati chafu za kuwania urais zinazolenga kuwaumiza kisiasa wale wanaotajwa kutaka kukiwania kiti hicho.
Huku Rais Kikwete akipambana kukinusuru chama chake na mpasuko uliojitokeza, hali si shwari kwenye serikali yake ambayo inakabiliwa na mdororo wa kiuchumi na kupanda kwa gharama za maisha.
Madaktari nchini wameuongezea machungu utawala wa sasa na wananchi kwa kuamua kugoma, wakiishutumu serikali wa kushindwa kuboresha mazingira yao ya kazi, vifaa, posho, mishahara, nyumba na huduma nyinginezo.
Mgomo huo uliodumu kwa takriban wiki moja sasa, unaelezwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii kuwa unaiweka serikali katika wakati mgumu wa kutawala.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, amesema kuwa serikali inakabiliwa na ukata mkubwa kiasi cha kushindwa kuwalipa wabunge waliokuwa kwenye vikao vya kamati mbalimbali kwa takriban siku tisa sasa.
Msigwa alitoa kauli hiyo jana mjini Kibaha alipokuwa kwenye mkutano wa hadhara ambapo alisema wabunge wanaishi kwa kukopa vyakula na malazi kwenye hoteli walizofikia.
“Serikali yenu imefilisika ndiyo maana inashindwa kutulipa, sasa niambieni mishahara ya walimu, madaktari na polisi wataitoa wapi?” alihoji.
Naye Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (Bavicha), John Heche, alisema serikali imewachoka wananchi wake na rais ameamua kwenda nchini Uswisi kuhudhuria mkutano wa kiuchumi wakati nchini kwake kuna mgomo wa madaktari.
No comments:
Post a Comment