tuwasiliane

Saturday, January 28, 2012

28 JAN. TUCTA waanzisha moto upyaaaaaa


Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limewasha moto mpya wa kutaka kima cha chini cha mshahara kiwe sh 500,000 badala ya kile ilichopendekeza mwaka juzi cha sh 315,000.

TUCTA imesema inataka kima cha chini kwa wafanyakazi kiwe sh 500,000 kwa kuwa gharama za maisha zimepanda maradufu ilhali kima cha chini kwa watumishi wa umma hakizidi sh 200,000.

Msimamo huo ulitolewa jana na Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Nicholaus Mgaya, alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa viongozi wa TUCTA, mkoa wa Dsm ambaye alisema mishahara ya wafanyakazi wa umma nchini ni midogo ukilinganisha na ile wanayolipwa wenzao wa nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Mgaya alisema mwaka juzi TUCTA ilitaka serikali kulipa kima cha chini cha sh 315,000 lakini sasa gharama za maisha zimepanda zaidi hivyo ni vema kikaongezeka na kuwa sh 500,000.

Alisema ni aibu kuzungumzia kima cha chini cha mshahara wa wafanyakazi wa umma hapa nchini kutokana na udogo wake ambao serikali haionekani kushtushwa na upandaji wa gharama za maisha ambao hauendani na kipato.

“Mishahara yetu ni midogo huwezi kumwambia mtu unapata sh 150,000 kwa kuwa ni aibu. Hata mshahara wa kima cha chini wa sh 315,000 tulioupendekeza Tucta wakati ule, hivi sasa umepitwa na wakati, hivyo mapendekezo yetu kima cha chini kiwe ni sh 500,000,” alisema.

Kwa mujibu wa Mgaya, hivi sasa maisha yanapanda kila kukicha, wenye nyumba nao hasa jijini Dar es Salaam wamekuwa wakipandisha kodi kila wakati bila kujali hali halisi ya maisha ya mwananchi wa kawaida.

Pia alisema kuwa, Tucta imelizingatia suala la kupanda kwa gharama za umeme na vitu vingine, hivyo utafiti unafanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu Mzumbe, ili kuwapatia hali halisi ya suala la uchumi nchini kabla ya kulizungumza.

SOURCE DARHOTWIRE

No comments:

Post a Comment