
WAKATI LEO michuano ya Mataifa ya Afrika, Afcon 2012, inaanza kutimua vumbi katika nchi za Guinea ya Ikweta na Gabon, timu ya Taiga ya Ghana inapewa nafasi kubwa ya kutwaa kombe hilo.
Kwa mujibu wa kura zilizopigwa na wasomaji wa mtandao wa goal.com, Senegal imetajwa kushika nafasi ya pili, huku Ivory Coast ikitwaa nafasi ya tatu.
Kura hizo zinaonesha kwamba, mshambuliaji wa kimataifa wa Senegal anayechezea klabu ya Newcastle inayoshiriki Ligi Kuu ya England, Demba Ba, ataibuka Mfungaji Bora.
Kiungo Andre Ayew wa Ghana ambaye ni mtoto wa gwiji, Abedi Pele, ametajwa kuwa ndiye atakayeibuka mchezaji bora chipukizi wa michuano hiyo.
Ghana mwaka 2010 ilishika nafasi ya pili baada ya kufungwa na Misri bao 1-0 katika fainali, michuano ikiwa imefanyika nchini Angola.
Michuano hiyo inashirikisha timu 16, huku timu za kundi A na B zikiwa kwenye miji ya Guinea ya Ikweta, Malabo na Bata, wakati miji ya Gabon ya Libreville na France Vile itakuwa na timu za kundi C na D.
Timu zinazoshiriki michuano hiyo ni Guinea ya Ikweta, Libya, Senegal, Zambia, Ivory Coast, Sudan, Burkina Faso, Angola, Gabon, Niger, Morocco, Tunisia, Ghana, Botswana, Mali na Guinea. Michuano hiyo itafikia tamati Februari 21 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment