
TIMU ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' inatarajia kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa na timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) 'The Leopards' Februari 23 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
DRC ndiyo imeomba kucheza mechi hiyo ya kirafiki dhidi ya Taifa Stars kwa kuwa itaweka kambi hapa Nchini kwa muda wa wiki moja kuanzia Februari 18 hadi 25 kwa ajili ya kujiandaa na mechi yao ya mchujo ya kuwania kushiriki Fainali za Kombe la Afrika (CAN) dhidi ya Mauritius.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania, Boniface Wambura alisema kuwa mechi ya DRC na Mauritius itachezwa Februari 29, nchini Mauritius, huku Stars yenyewe itacheza mechi ya kwanza ya mchujo kwa ajili ya fainali hizo za Kombe la Afrika (CAN) 2013 zitakazofanyika Afrika Kusini dhidi ya Msumbiji.
Alisema kutokana na timu ya Misri kuomba kucheza na Stars tarehe kama hizo wanafanya mawasiliano na Misri kuona kama wanaweza kusogeza mbele au kurudisha nyuma na kama haitawezekana wapeleke timu ya vijana kucheza na Misri.
"Tuna mashindano makubwa mbele yetu tunahitaji mechi nyingi za kirafiki hivyo hatutaki kuzikosa, tutaongea na Misri kama wanaweza wasogeze mbele au warudishe nyuma ikishindikana kabisa tutawaomba tupeleke timu ya vijana," alisema Wambura.
Mwezi Mei, 2009 Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) ambao walikuwa mabingwa wa Afrika wa michuano ya wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) ambazo pia Tanzania ilishiriki, walicheza mechi ya kirafiki ya kimataifa na Taifa Stars na kuilaza mabao 2-0 katika uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Walikuwa DRC ambao walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya tano, lililofungwa na Kaluyituka Dioko baada ya mabeki wa Stars kujichanganya katika kuokoa mpira wa kona. Katika kipindi cha pili Kaluyituka aliwaduwaza tena Watanzania kwa kufunga bao la pili.
Katika viwango vya Shirikisho la Soka Kimataifa FIFA, timu ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) inashika nafasi ya 125 huku Tanzania ikishika nafasi ya 137.
Kihistoria DRC ndiyo timu ya kwanza katika Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 1974, na pia imewahi kutwaa ubingwa wa Kombe la Afrika (CAN) mara mbili, ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1968 na mara ya pili mwaka 1974.
DRC inaundwa na nyota wengi wanaotokea katika klabu ya TP Mazembe kama Miala Nkulukutu, Joel Kimwaki, Bedi Mbenza, Eric Bokanga na Tresor Mputu, kinanolewa na kocha Claude Le Roy.
Kocha wa Taifa Stars, Jan Poulsen anatakiwa kuhakikisha kikosi chake kinapata ushindi katika mechi hiyo ili kuweza kurudisha imani kwa mashabiki wa soka wa Tanzania ambao wanaipenda Taifa Stars ila imekuwa ikiwakitisha tamaa mara kwa mara.
Taifa Stars imewahi kushiriki mara moja Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) mwaka 1980, lakini haijawahi kushiriki fainali za Kombe la Dunia na imekuwa ikitolewa katika hatua za awali katika harakati zote za kufuzu michuano hiyo.
No comments:
Post a Comment