tuwasiliane

Monday, January 2, 2012

02 JAN. Jengo la Simba kuvunjwa


SIMBA imesema italibomoa jengo lake lote la sasa kutokana na kutokidhi viwango vya ujenzi ambapo haiwezekani kuongezwa tena kwa zaidi ya ghorofa nane.

Akizungumza jijini jana Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismaili Aden Rage alisema mara baada ya kulibomoa jengo hilo watajenga lingine la kati ya ghorofa 12 au 15.

Alisema awali walikuwa wakijua wangeweza kuendelea kujenga kwenye jengo lao sasa, lakini kwa mujibu wa mkandarasi wao jengo hilo haliwezi kuongezewa zaidi ya ghorofa nane.

Alisema michoro ya jengo hilo jipya tayari ipo na wako mbioni kuingia mikataba na benki mbalimbali kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa ghorofa lao jipya unaotarajiwa kuanza mwezi huu.

Hata hivyo, Rage alifafanua kuwa jengo litakalovunjwa ni lile jipya maarufu kama Jengo la Kitega Uchumi ambalo lipo pembeni ya jengo lao la klabu mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam.

Pia Rage alisema Simba imepata kibali cha kumiliki kiwanja chake eneo la Bunju Dar es Salaam, ambalo watajenga uwanja wa kisasa wa soka.

Alisema wamepewa kibali hicho wiki iliyopita na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na sasa wanatakiwa kulipia shilingi milioni 85 ili waumiliki
uwanja huo.

Alisema kati ya fedha hizo wanazodaiwa tayari wamelipa Sh milioni 50 na kudai kuwa kabla ya miezi sita waliyopewa kulipia uwanja huo haijafika watakuwa tayari walishalipa deni hilo.

Alisema kutokana na kukosekana kwa kibali hicho ndio maana walikuwa wazito kutoa taarifa za ujenzi wa uwanja wao kwani wasingeweza kuanza ujenzi bila ya kuwa na kibali hicho.

Rage alisema hata wadhamini wa ujenzi wa uwanja wao kutoka Uturuki walikuwa wajanja kwani walikataa kuanza ujenzi wa uwanja huo mpaka wakione kibali hicho.

“Hawa Waturuki walikuwa wajanja hawakutaka kuanza ujenzi mpaka waone kibali, sasa tumeshapata kibali hicho ujenzi utaanza mara moja,” alisema Rage.

Wakati huohuo, Simba imesema itamuadhibu mshambuliaji wake wa kimataifa kutoka Uganda, Emmanuel Okwi kutokana na kushindwa kujiunga kwenye kambi kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema jana kuwa lazima wamuadhibu mshambuliaji huyo kutokana na kitendo chake cha kushindwa kujiunga na wenzake.

Alisema walimpa Okwi ruhusa ya wiki mbili kwenda kupumzika nyumbani kwao Uganda, ambazo tayari zimekwisha huku wakiwa hawajui nini kimemsibu mchezaji huyo.

Hata hivyo, Kaburu alisema watampa nafasi mchezaji huyo kujitetea kabla hawajakimbilia kutoa adhabu kwa sababu anaweza kuwa na sababu za msingi za kuchelewa kwake.

Alisema kwa kawaida mchezaji hukatwa dola 700 kutoka sehemu ya mshahara wake kwa kosa kama hilo na kusisitiza kuwa hayo yote yatategemea na jinsi atakavyoeleza sababu za
kuchelewa kwake.

Kutokana na kushindwa kujiunga na kambi ya timu hiyo, Okwi hayumo kwenye kikosi cha Simba kitakachoshiriki Kombe la Mapinduzi ambalo litaanza leo kwenye uwanja wa Amani,
Zanzibar.

No comments:

Post a Comment