
MSHAMBULIAJI wa Manchester City, Mario Balotelli ameingia katika kashfa nyingine baada ya kutibuana na mchezaji wa timu yake Micah Richards wakati wa mazoezi ya timu hiyo.
Wachezaji hao wawili walitibuana mwishoni mwa mazoezi na kuamuliwa na wachezaji wengine wa timu hiyo wakati walipokuwa katika mazoezi wakijiandaa na mechi ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Arsenal siku ya Jumapili.
Watu walioshuhudia tukio hilo wanasema wachezaji hao wawili walitupiana maneno kabla ya kutaka kushikana huku Richard akionekana kuchukizwa na kilichozungumzwa na Balotteli.
Hata hivyo, Richards ameibuka na kusema kwamba suala hilo wameishalimaliza,"mimi na Mario tupo vizuri, mambo ya kutofautiana hutokea mazoezini, huwa tunapeana mikono baada ya hapo, huonyesha kila mmoja anamjali mwenzake,"alisema Richards kwenye mtandao wa Twitter.
Hilo siyo tukio la kwanza wachezaji kutofautiana katika klabu ya City kwani tukio kama hilo liliwahi kutokea mwaka uliopita ambapo Balotelli alitibuana na Jerome Boateng na Vincent Kompany wakati Emmanuel Adebayor na Kolo Toure waliwahi pia kutibuana.
Tukio hili linaingia katika matukio mbalimbali yaliyomtokea Balotelli na kufanya kuwa gumzo kuliko uchezaji wake uwanjani kwa sababu nyumba yake iliwahi kuungua na kutangazwa sana, pia wiki hii zilitoka taarifa kwamba mshambuliaji huyo alionekana mitaani kabla ya City kukutana na Chelsea ingawa kocha wa City, Rberto Mancini alikanusha taarifa hiyo.
Ukiacha matukio hayo, Balotelli amekuwa na msimu mzuri uwanjani kwa sababu mpaka hivi sasa ameishafunga mabao 11.
No comments:
Post a Comment