
WAKATI Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Charles Boniface Mkwasa akidai tayari ameishawasilisha ripoti yake ya mashindano ya Chalenji kwa Shrikisho la Soka Tanzania (TFF), Shirikisho hilo limesema bado halijaipokea ripoti hiyo.
Hali hiyo imezua mkanganyiko na maswali mengi miongoni mwa wapenzi na mashabiki wa soka nchini ambao wana hamu kubwa ya kutaka kujua nini kilichosababisha Kilimanjaro Stars kufanya vibaya katika mashindano ya Chalenji ikiwa ni pamoja na mapendekezo ya kocha huyo juu ya nini cha kifanyike kwa faida ya soka la Tanzania.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mkwasa alisema tayari ameishawasilisha TFF ripoti yake hiyo na kuongeza kuwa hivi sasa ni jukumu la shirikisho hilo kuipitia na kuifanyia kazi.
"Tayari nimeishawasilisha ripoti hiyo ya mashindano ya Chalenji tangu jana (Juzi) na sasa ni jukumu la TFF kuifanyia kazi.
"Hata hivyo watu wengi wamekuwa wakiniuliza maswali mengi, lakini nachotaka kusema ni kwamba mimi siyo mtoaji wa hukumu kwa yale yote yaliyojitokeza katika mashindano hayo," alisema Mkwasa.
Alisema TFF ndiyo yenye kazi hiyo isipokuwa yeye kazi yake ni kutoa ripoti ya yale yote yaliyojitokeza katika mashindano hayo na siyo kutoa hukumu.Hata hivyo Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alipoulizwa kama tayari wameshaipokea ripoti hiyo ya Mkwasa alisema kuwa bado hawajaipata.
"Bado hatujaipata na kama ikifika tutawajulisha," alisema Wambura.
Wapenzi wa soka hapa nchini wanasubiri kujua maoni ya kocha huyo pamoja na benchi lake la ufundi juu ya nini kilichosabibisha Kilimanjaro Stars ishindwe kufanya vizuri kwenye mashindano ya Chalenji yaliyokuwa yakifanyika hapa nchini, Uganda ilinyakua Kombe hilo.
Katika Mashindano hayo Kilimanjaro Stars ilionyesha kiwango cha chini jambo lililosabibisha baadhi ya mashaki kuanza kuizomea kila ilipokuwa ikitinga uwanjani.
No comments:
Post a Comment