
WACHEZAJI wa timu Taifa, Kilimanjaro Stars bado wanaendelea kusotea ahadi ya shilingi 10milioni iliyotolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda mwezi mmoja uliopita kama hamasa ya timu hiyo kufanya vizuri kwenye mechi ya awali kuwania kufuzu kucheza hatua ya makundi Kombe la Dunia dhidi ya Chad.
Waziri Pinda alitoa ahadi hiyo wakati wa hafla ya kuiaga Stars kwenye Hoteli ya Newafrica jijini Dar es Salaam, Novemba 7 tayari kwa safari ya kwenda Chad, ambapo ilishinda mechi ya kwanza kwa mabao 2-1.
Katika hafla hiyo iliyoshuhudiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo (BMT), Dioniz Malinzi na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Pinda alikaririwa akisema: "Naamini wengi mnafahamu timu yetu ina mtihani mkubwa wa kucheza na Chad Ijumaa wiki hii, na marudiano Novemba 15. Nimeona na mimi nitoe motisha kwa wachezaji ili wafanye vizuri," alisema Pinda.
"Naomba makampuni, taasisi, watu binafsi na mashirika mbalimbali waisapoti timu yetu kwa hali na mali kwa wote wanaoitakia heri Tannzania."Nimempa jukumu Waziri mwenye dhamana ya michezo (Emmanuel Nchimbi) kuhakikisha michango yote inapita kwake na inawafikia walengwa."
Hata hivyo baadhi ya wachezaji wameiambia Mwananchi jana kuwa, mpaka leo ahadi hiyo haijatekelezwa na hawajui lini itatekelezwa."Kwanza tunamshukuru Waziri Mkuu kwa moyo wake wa hamasa kwetu, kweli tulijituma na kupata ushindi ugenini," alisema mmoja ya wachezaji ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini.
"Lakini tunashangazwa na ukimya huu, yaani mpaka leo hatujapewa mgao wa hizo pesa, na mbaya zaidi hakuna taarifa za nini kinaendelea," alisema."Wakati fulani tulipozwa kwa kuambia utaratibu wa kuzipata pesa hizo huchukua muda mrefu kwa vile zinapita sehemu nyingi."Sasa, niulize juzi tu hapa posho za wabunge zimepandisha fasta na chini ya mwezi mmoja wakaanza kulipwa, sisi tu hii hizi 10milioni ni mwezi sasa."
Awali, Mwandishi wa Habari wa Waziri Mkuu, Irene Bwire, alisema Waziri Mkuu alikwishaagiza fedha hizo zitolewe Hazina kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kwa ajili ya wachezaji hao.
"Dodoso imekwishaandikwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo kwa utekelezaji, sasa sifahamu kilichoendelea huko," alisema Bwire.
Hata hivyo wakati wachezaji wakilalamikia mgao huo, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah aliiambia Mwananchi jana kuwa, fedha hizo si kwa ajili ya mgao wa bali ni kutunisha mfuko wa kusaidia maendeleo ya timu ya taifa.
"Tunachofahamu ahadi ya Pinda ni sehemu ya ushawishi ili kuwavuta wadau wengine kuchangia timu ya Taifa na kuipa motisha ya kufanya vizuri katika michuano mbalimbali.
"Ni kweli fedha hizo hazijafika TFF, sababu za kuchelewa mpaka sasa sifahamu na si wajibu wangu kujibu hilo, waulizwe Wizara Michezo na Utamaduni," alisema Osiah.Aliongeza: "Inawezekana kweli zimechelewa, lakini hata kama zingewahi kutoka lengo si kuwagawia wachezaji bali kutunisha mfuko wa kusaidia timu kufanya vizuri.
Mwananchi ilipomtafuta Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo Emmanuel Nchimbi, simu yake ya kiganjani haikuwa na majibu, wakati Katibu wake Seth Kamuhanda haikupatikana kabisa.
Alipoulizwa Mkurugenzi wa Michezo Nchini, Leonard Thadeo alijibu kwa ufupi: "Sina cha kukujibu sasa, sifahamu lolote, ngoja nifuatilie kesho (leo) nitakupa majibu."
No comments:
Post a Comment