tuwasiliane

Wednesday, December 14, 2011

14 DEC.CECAFA YAPATA HASARA MICHUANO YA CHALLENGE


MICHEZO 26 ya michuano ya 35 ya Kombe la Chalenji iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwaka
huu imeingiza kiasi cha Sh 267,066,000.

Michuano hiyo ilianza Novemba 25 hadi Desemba 10, ambapo timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ iliibuka bingwa.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa hatua ya makundi ya michuano hiyo iliingiza Sh 145,613,000, robo fainali (Sh 58,470,000), nusu fainali (Sh 55,787,000) wakati fainali iliingiza Sh 17,196,000.

Kila siku zilichezwa mechi mbili isipokuwa Novemba 26 mwaka huu ambapo ilikuwa siku rasmi ya ufunguzi na Novemba 28 mwaka huu zilichezwa mechi tatu katika mashindano hayo yaliyoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Ccecafa) na
kushirikisha timu za mataifa 12.

“Mechi iliyoingiza fedha nyingi kuliko zote ilikuwa ya ufunguzi hatua ya makundi kati ya Tanzania na Rwanda ambapo zilipatikana Sh 64,178,000 wakati fedha kidogo (Sh 446,000) zilipatikana kwenye mechi kati ya Uganda na Somalia iliyochezwa Novemba 28 mwaka huu
Uwanja wa Azam.

“Jumla ya mashabiki walioshuhudia michuano hiyo walikuwa 103,312. mashabiki walioshuhudia hatua ya makundi walikuwa 65,617, robo fainali (17,844), nusu fainali (16,014) wakati fainali walikuwa 4,837.

“Mechi iliyokuwa na mashabiki wengi zaidi ni kati ya Tanzania na Rwanda ambapo waliingia 23,946 wakati iliyoingiza wachache ni 446 walioshuhudia mechi kati ya Somalia na Uganda,” alisema Wambura.

Mwamko wa mashabiki uwanjani kwenye mashindano hayo mwaka huu ulikuwa mdogo ukilinganisha na mwaka jana, hali ambayo ilichangia mapato kidogo na hiyo ni kutokana na
timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kutofanya vizuri kwenye mechi zake.

No comments:

Post a Comment