
TIMU ya soka ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ leo itashuka dimbani dhidi ya Rwanda ‘Amavubi’ kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Mechi hiyo itakayoanza alasiri itatanguliwa na ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya timu ya soka ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ na Sudan itakayoanza saa saba mchana.
Rwanda iliyokuwa kundi A na timu za Kilimanjaro Stars, Zimbabwe na Djibouti imeingia hatua hiyo ikiwa imeshinda mechi zake zote.
Iliifunga Kilimanjaro Stars bao 1- 0 kwenye mechi ya ufunguzi, kisha ikaifunga Djibouti mabao 3-0 kabla ya kuifunga Zimbabwe mabao 2-0 na kutinga hatua ya robo fainali ambapo iliifunga Zanzibar mabao 2-1 na kuingia fainali kwa kuifunga Sudan mabao 2-1.
Uganda iliyokuwa Kundi B na Zanzibar, Somalia na Burundi ilishinda mechi zote isipokuwa moja tu iliyofungwa bao 1-0 na timu Burundi.
Kama rekodi ya matokeo ya mechi zilizopita kwenye mashindano haya zina nafasi kwenye
mchezo wa soka basi ni fainali rahisi sana kwa Rwanda kwani yenyewe imeingia hatua hiyo kwa kupata ushindi wa asilimia 100.
Lakini mchezo wa soka ni zaidi ya historia ya nini timu hizo zilifanya kwenye mechi zake zilizopita, uwezo, maandalizi na nidhamu ya mechi yenyewe inaweza kubadilisha kibao cha matokeo ya mchezo wenyewe.
Uganda tokea mashindano haya yaanze inaonekana kucheza kitimu zaidi ikitegemea ubora wa kikosi cha timu hiyo kilichokaa pamoja kwa muda mrefu zaidi huku Rwanda inayocheza mpira wa nguvu na kasi ikitegemea uzoefu wa kocha wao Sredojovic Milutin’ Micho’ kwa soka la ukanda huu.
Mabingwa wa mwaka jana Kilimanjaro Stars nao watapata nafasi ya angalau kuibuka na dola 10,000 kama itaibuka mshindi wa tatu lakini Sudan nayo sio timu ya kubeza hivyo Stars haina budi kukaza buti.
No comments:
Post a Comment