
SARE ya mabao 3-3 waliyopata vinara wa Ligi Kuu Bara, Simba dhidi ya Moro United katika mechi ya kufunga duru la kwanza msimu huu, imezaa 'faida' kwa mabingwa watetezi Yanga ambao ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Dodoma, mjini Dodoma umewafanya kuendelea kuwa nyuma tofauti ya pointi moja tu.
Zaidi ya mwezi mmoja na nusu sasa, mabingwa watetezi Yanga walikuwa nafasi ya mbali katika msimamo wa ligi, ikiwa ni mara ya kwanza kushika nafasi katika kipindi cha zaidi ya miaka 20.Vinara Simba wakiwa bado 'wamelainishwa' na kipigo cha bao 1-0 toka Yanga Jumamosi iliyopita, ililazimika kutumia nguvu nyingi kukomboa mabao wawili na kufanya matokeo kuwa 3-3, baada ya kuwa nyuma kwa mabao 3-1 hadi kumalizika nusu ya kwanza.
Pamoja na sare hiyo, Simba watabaki kileleni mwa msimamo hadi katikati ya Januari mwakani ligi hiyo itakapoanza mzunguko wa pili. Wamefikisha pointi 28, Yanga wakiwa na pointi 27 baada ya michezo 13 kila mmoja.
Azam wanaoshika nafasi ya tatu, wametoka sare ya 1-1 na Toto kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na kufikisha pointi 22.
Shujaa wa mechi ya Yanga alikuwa mshambuliaji wa kimataifa wa Ghana Kenneth Assamoah aliyefunga bao pekee katika dakika ya 44 akimalizia kazi nzuri Hamis Kiiza.Ushindi wa Yanga walioweka rekodi ya kuwa timu pekee kuifunga Simba mpaka duru la kwanza linamalizika, hakuwa rahisi kwani walikamiwa sana na wapinzani wao.
Mwishoni mwa mechi hiyo kwenye Uwanja wa Jamhuri, mashabiki wa Polisi waliingia uwanjani na kutaka kumpiga mwamuzi kwa madai ya kuibeba Yanga, ikiwa ni pamoja na kukataa bao lao la kusawazisha la dakika ya 85 kupitia kwa Juma Semsue, ambaye mwamuzi alidai alikuwa ameotea.
Kocha msaidizi wa Yanga, Fred Minziro mara baada ya mechi hiyo alisema kwa ufupi: "Umoja na mshikamano ndio uliowapa ushindi kwenye mechi hiyo.
Timu zote zilishambuliana kwa zamu, huku mabingwa Yanga, wakionekana kung'ara zaidi hasa sehemu ya kiungo, na Polisi wakicheza vizuri katika safu yao ya ulinzi.
Kocha wa Yanga Costadin Papic alilazimika kukaa jukwaani kushuhudia mechi hiyo badala ya kukaa kwenye benchi kama ilivyokuwa kwenye mechi dhidi ya watani wao Simba Jumamosi iliyopita kwa kuwa hana kibali cha kufanyia kazi.
Kwenye Uwanja wa Chamazi, iliwachukua Moro United dakika mbili tangu kuanza kwa mchezo kulifikia lango la Simba na kutumia vizuri mwanya wa kuchelewa kujipanga kwa mabeki wa Wekundu hao wa Msimbazi kufunga bao la kuongoza kupitia kwa Andrew Kasemba aliyeunganisha wavuni krosi ya Lambele Jerome.
Mungusa alikosa bao la wazi lakini alirekebisha makosa yake na kuifungia Simba bao la kusawazisha robo saa baadaye, akiruka juu na kuukwamisha mpira wavuni kufuatia kona ya Salum Machaku.
Bao hilo la Simba lilikuwa kama 'limechokonoa' kiu ya mabao kwa Moro United, kwani dakika ya 43 juhudi binafsi za Kasembe zilizaa bao la pili baada ya kuwalamba chenga mabeki wa Simba na kipa Juma Kaseja kabla ya kukwamisha mpira wavuni.
Wakati bado mashabiki wa timu ya Simba iliyokuwa chini ya kocha Richard Amatre akichukua nafasi Moses Basena, wakijiuliza kulikoni, Moro United walirejea tena kwenye kamba za Msimbazi na kupachika bao la tatu.
Bao hilo lilitumbukizwa wavuni na kinara wa mabao Gaudence Mwaikimba dakika za nyongeza kuelekea mwishoni mwa kipindi cha kwanza na kufanya matokeo kuwa 3-1 mpaka mapumziko.
Simba waliocheza mechi hiyo wakiwa na vitambaa vyeusi mkononi kuomboleza msiba wa mama mzazi wa kocha wao Moses Basena walirudi kipindi cha pili na nguvu mpya na kufanya mashambulizi mengi langoni mwa Moro United.
Kuingia kwa Gervais Kago na Jonas Gerald wakichukua nafasi za Ulimboka Mwakingwe na Mwinyi Kazimoto, kulileta uhai na kujipatia mabao mawili, moja likifungwa na Kago kwa shuti la mita 25 dakika ya 76, na kisha matokeo kuwa 3-3 kufuatia mpira wa adhabu ndogo wa Salum Machaku kwenda moja kwa moja wavuni. Moro walimaliza mchezo wakiwa pungufu baada ya mwamuzi Israel Nkongo kumtoa nje kwa kadi nyekundu Salum Telela kutokana na mchezo mbaya dhidi ya Gelard.
Makamu mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alinusurika kupigwa na mashabiki wa Simba wakimtuhumu kuharibu timu yao, kabla ya askari waliokuwa uwanjani kuzima vurugu hiyo.
Hii ni sare ya pili kwa idadi hiyo ya magoli kwa Simba, ambapo sare ya kwanza waliipata kwenye mechi waliyonusurika kipigo na Toto African ya Mwanza.
Kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola alisema wachezaji wake hawakucheza vizuri kutokana na kuwa 'vibaya kisaikoloji' tangu kipigo cha Yanga.
Naye kocha wa Moro United, Hassan Banyai aliwasifu wachezaji wake kwa kuonyesha uwezo mkubwa, lakini alisema mabeki wake walijisahau kipindi cha pili na kutoa nafasi kwa Simba kufunga mabao mawili.
Katika mechi ya iliyowakutanisha maafande watupu, JKT Ruvu na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Mjini Arusha, Oljoro JKT iliilaza Villa Squad bao 1-0, mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid huku Mtibwa Sugar na Azam zikitoka sare ya 2-2 kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani.
No comments:
Post a Comment