
UCHAGUZI Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki, Cecafa unafanyika leo kwa kiongozi wa sasa Leodegar Chilla Tenga akitetea kiti chake huku Fadou Hussein akinyemea kiti hicho.
Kazi kubwa inaweza kumkuta Tenga akiwania kiti hicho, kwani kila upande unategemea ushawishi kwa wajumbe wa Ukanda wa Cecafa kutoka mataifa 11. Uchaguzi huo unafanyika kwenye Hoteli ya JB Belmont jijini Dar es Salaam.
Moja ya ajenda katika mkutano huo utakaonza saa 4.00 asubuhi ni uchaguzi wa Kamati mpya ya Utendaji ya Cecafa ambao unajumuisha nafasi za mwenyekiti na wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji.
Mbali na nafasi hiyo, nafasi nne za Kamati ya Utendaji zinazowaniwa na Abdiqani Saeed Arab (Somalia), Tariq Atta Salih (Sudan), Justus Mugisha (Uganda), Tesfaye Gebreyesus (Eritrea), Hafidh Ali Tahir (Zanzibar), Sahilu Wolde (Ethiopia), Raoul Gisanura (Rwanda) na Abubakar Nkejimana kutoka Burundi.
Wakati huo huo, timu zinazoshiriki michuano ya Chalenji, zimeanza kuwasili na tayari Zanzibar, Rwanda, Sudan, Uganda, Somali na Djibouti zimeshatua nchini wakati inayotarajiwa kuwasili leo ni Ethiopia huku Kenya na Malawi zikitarajiwa kuwasili Jumatatu.
No comments:
Post a Comment