tuwasiliane

Wednesday, November 23, 2011

23 NOV.Namibia yajitoa tusker challenge cup


NAMIBIA imeutupa mwaliko wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati, Cecafa kushiriki mashindano yake kwa kile ilichoeleza kuwa wako na ratiba ngumu na pia mashindano hayo hayako katika kalenda ya Shirikisho la Kimatafa la Soka, Fifa.

Kwa mujibu wa gazeti la Namibian, Chama cha Soka Namibia, kimesema pia kuwa endapo wataamua kutengeneza timu ya taifa, watakuwa wamevuruga mwenendo wa ligi hiyo.

Kocha wa timu hiyo, Brave Warriors, Tim Isaacs alisema kuwa kutokana na michuano hiyo kupangwa katikati ya ligi yao Novemba 25 hadi Desemba 10, hawatoweza kutengeneza timu ya taifa ambayo inaundwa zaidi na wachezaji wa ligi za ndani.

Isaacs alisema pia kuwa wamekwishawapelekea taarifa za kujitoa kwao kwenye michuano hiyo."Kwa bahati mbaya hatutashiriki michuano hii kwa sababu hatutaki kuvuruga program zetu," alisema Isaacs.

"Tunmeshawasiliana na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah kumweleza kuwa hatutaweza kushiriki."

Namibia, ilikuwa ichukue nafasi ya Eritrea ambayo imejitoa kwenye michuano hiyo kutokana na ukata. Timu hiyo ilipangwa kufungua dimba na Djibouti katika mechi ya Kundi A Novemba 27.Hata hivyo, Isaacs aliliambia pia gazeti la Namibian Sport kwamba Namibia iko katika maandalizi kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Angola Desemba 23.

"Pambano lipo kama kawaida," Isaacs alisema. "Pia tunajaribu kutafuta mechi nyingine kabla ya kumalizika kwa msimu. Bado tuko katika mazungumzo."

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Boniface Wambura alisema kuwa Musonye ndiye anayeweza kulizungumzia suala hilo.Mwananchi ilipomtafuta Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholaus Musonye, alisema kuwa wamealika timu nyingi na nyingi zimeonyesha nia ya kutaka kushiriki mashindano hayo. hata hivyo hakutaka kutaja moja kwa moja nchi iliyoonyesha nia.

No comments:

Post a Comment