SIMBA iliyotulia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi zake 18, imeukimbia Uwanja wa Sigara ilipokuwa ikifanya mazoezi na sasa imetua Kinesi, jijini Dar es Salaam lakini uongozi umetangaza rasmi 'Operesheni Mechi Tano.'
Wekundu hao wameondoka Sigara maeneo ya Chang'ombe, Dar es Salaam ambako pia African Lyon wanayokwaana nayo Oktoba 16 inautumia. Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' aliiambia Mwanaspoti jana Jumatatu kuwa; "Tumeanzisha operesheni maalumu tumeipa jina la "Operesheni Mechi Tano' itamhusisha kila Mwanasimba popote kuhakikisha kwamba tunashinda mechi zote tano zilizosalia mzunguko wa kwanza tena kwa kishindo, hiyo ndiyo operesheni ya uhakika baada ya hapo tunatulia tunasubiri mzunguko wa pili kwa raha zetu."
Simba inakabiliwa na mechi tano dhidi ya African Lyon, Ruvu Shooting, JKT Ruvu, Yanga na Moro United.
Simba inaendelea na mazoezi hayo kwa kuwatumia wachezaji 17 isipokuwa Juma Jabu, Juma Kaseja, Juma Nyosso na Victor Costa walioko Taifa Stars, Ulimboka Mwakigwe amefiwa na baba yake mdogo na Haruna Moshi �Boban� anauguliwa na mwanaye.
Kati ya waliofika ni Mnyarwanda, Patrick Mafisango ambaye awali, alisimamishwa na uongozi wa klabu hiyo baadaye akasamehewa na Salum Machaku aliyeondolewa bandeji gumu wiki iliyopita, Gervais Kago wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Mzambia Felix Mumba Sunzu.
Meneja wa Simba, Abdalah King Kibaden alisema kuwa ; "Tumeanza mazoezi kama kawaida, tumeamua kuhama uwanja kwavile tulikuwa tunabanana na African Lyon, tumeona bora tuhamie Kinesi ni uwanja wetu pia tutapata nafasi zaidi."
Kocha Mkuu Moses Basena aliwasili jana Jumatatu, lakini msaidizi wake, Richard Amatre alisema mazoezini kuwa; "Nimekazania sana mazoezi kwa sababu nataka wachezaji wangu wawe na stamina na hiyo itawasaidia kucheza muda mrefu uwanjani, nguvu za miguu kitu ambacho wengi wao walikuwa hawana.
�Nataka turudi kivingine kwenye ligi baada ya haya mapumziko, na tumepania kucheza mpira wa ufundi zaidi, nguvu na kumuhimili kila mmoja tutakayekutana naye, tutakuwa tunabadilika kila mechi kulingana na timu tutakayokutana nayo ndio maana nataka wachezaji wangu wawe fiti kuliko kawaida,�alisisitiza kocha huyo huku akisema ubora wa viwanja wanavyotumia kuwa ni duni.
Daktari wa timu hiyo Abeid Shindika aliiambia Mwanaspoti kuwa Amir Maftah ameanza mazoezi mepesi na ana asilimia kubwa ya kucheza dhidi ya African Lyon Oktoba 16.
source
© Mwananchi Communications Ltd:2007
No comments:
Post a Comment