tuwasiliane

Monday, October 10, 2011

Kocha awaomba msamaha Waganda

KAMPALA, Uganda
KOCHA wa timu ya Taifa ya Uganda, Bobby Williamson amewaomba msamaha mashabiki wa soka wa Uganda baada ya timu yake kusndwa kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika 2012.

Hakuna mchezaji wa Uganda hata mmoja aliyekuwa na moyo wa kutoka kwenye vyumba vya kubadilishia nguo juzi kwenye uwanja wa Namboole baada ya timu yao kutoka sare ya 0-0 na Kenya na hivyo kushindwa kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika 2012.

Hivi sasa Uganda itabidi isubiri mwaka mmoja mwingine ili iweze kutafuta nafasi ya kufuzu kushiriki Fainali za Afrika zitakazofanyika 2013.Wachezaji wengi wa Uganda walikuwa wakilia na kuhuzunika huku wakishindwa kuamini kilichowatokea ndani ya dakika 90 zac mchezo wakati walitakiwa kushinda ili wafuzu.

Kocha wa Uganda, Bobby Williamson ambaye alitua nchini humo miaka mitatu iliyopita akiwa na kauli ya kuhakikisha Uganda inafuzu fainali za Afrika, pia alishindwa kuamini kilichotokea.

"Nawatakia Angola fainali bora za Afrika,"Bobby Williamson.

"Siwezi kujadili hali yangu ya baadaye hivi sasa, ila nipo Uganda kwa ajili ya soka ya Uganda ambapo naamini nimeweza kuibadilisha,"alisema Bobby Williamson.

"Nawashukuru mashabiki waliojitokeza kwa idadi kubwa na nawaomba msamaha, pia namshukuru raisi na nawashukuru mawaziri na wabunge kwa kujitokeza," alisema Bobby Williamson.

Alisema,"mimi ninapenda kufanya kazi ya soka na ninapenda kufanya kazi na waganda, ninaamini nitaendelea kuwapo mpaka Shirikisho la Soka la Uganda litakaponiambia halinihitaji."

"Mbio zetu za kuwania kufuzu kushiriki fainali za Afrika zilikuwa nzuri, tunao mashabiki wazuri na tunao wachezaji ambao wanafunga magoli, ninawasikitikia vijana wangu ambao walijitahidi sana katika harakati zetu za kuwania kufuzu, lakini juhudi zao zimeshindikana dakika za mwisho,"alisema Bobby Williamson.

Naye kocha wa timu ya Taifa ya Kenya, Zedekiah Otieno alisema,"Waganda wenyewe itabidi wajilaumu, walipata nafasi nyingi, lakini walishindwa kuzitumia."

Wachezaji Brian Umony, Moses Oloya, Mike Sserumaga, Geoffrey Massa wote walipata nafasi za kuifungia Uganda, lakini hawakuzitumia vizuri.

Saa 24 kabla ya mechi hiyo kocha Bobby Williamson alimtimua mshambuliaji hatari wa Uganda, David Obua kwenye timu kwa kile alichodai ukosefu wa nidhamu.

Kabla ya mechi kitendo hicho hakikoonekana na madhara, lakini baada ya mechi mashabiki wa Uaganda walianza kumlaumu Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Uganda FUFA kwa kukubali mchezaji huyo kutimuliwa kwenye kikosi.

Kitendo cha kutimuliwa Obua kilichukuliwa na mashabiki kwamba ndiyo sababu kubwa iliyofanya Uganda kushindwa kushinda mechi hiyo.Wakati huo huo timu kubwa zilizoshindwa kufuzu mpaka sasa ni Nigeria, Afrika Kusini, Misri, Cameroon.

Timu ambazo tayari zimeishafuzu ni Zambia, Ghana, Guinea, Angola, Senegal, Mali, Burkina Faso, Niger, Ivory Coast, Botswana, Tunisia wakati Libya ina uhakika wa kupata nafisi ya kufuzu ikiwa timu ambayo imefanya vizuri na kushika nafasi ya pili.

No comments:

Post a Comment