
Aliyekuwa kipa wa zamani Juma Pondamali
JUMA PONDAMALI MENSAH: Kipa aliyefungiwa mara tano na
mara nne mapambano yalivunjika
KENNEDY MWAISABULA
WAPO makipa kama Peter Manyika, Chachala Muya, Kichochi Kilembe, Abdul Kipenga, Spear Mbwembwe, Issa Manofu na wengineo walitaka kumuiga Juma Pondamali Mensah kwa vituko na mbwembwe zake akiwa langoni, lakini hawakufikia hata robo yake.
Pondamali alikuwa ni wa aina ya kipekee ndani ya nchi hii , ambaye kwa sasa ndio anaowanoa makipa takribani wote wa Taifa Stars akimsaidia Mdenmarki, Jan Poulsen.
Pondamali ambaye alizaliwa mwaka 1957 jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya Ocean Road, elimu yake ya msingi aliipata Mlimani na baadaye Karume kabla ya elimu yake ya Sekondari kuipata Mzizima na muda wote huo wa utoto wake soka likiwa ndani ya damu yake.
STANCULESCU VICTORIA AITA WENYE VIPAJI JANGWANI
Kocha raia wa Romania, Victor Stanculescu mwanzoni mwa miaka ya 70 baada ya kuona wachezaji wa Yanga umri wao unasogea aliita watoto wote wenye vipaji wenye umri wa Kids yaani miaka 14 na 15 ili waje wachukue nafasi za wakongwe na ndipo walipojitokeza watoto takribani mia na kupatikana wachache akina Mohamed Mkweche, Adolf Richard, Kasimu Manara, Mohammed Tostao, Gordian Mapango na Juma Pondamali na wengineo ambao kwa maelezo ya Victor aliwatabiria kuwa wote lazima watacheza timu ya Taifa na ndicho hatimaye kilitokea. Pondamali na wenzake walipandishwa hadi kikosi cha pili na baadaye mwaka 1974 walipandishwa hadi kikosi cha kwanza na Pondamali akiwa kipa wa tatu akifuatiwa na wakongwe Muhidini Fadhili na Elias Michaek na kutengeneza muziki mzito ndani ya vijana wa Jangwani na walifanya vizuri mwaka 1974 kwa kuwafunga mahasimu wao na mwaka uliofuatia kuchukua ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati na balaa lilitokea katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika na kutolewa na Enugu Rangers ya Nigeria.
NINI CHANZO CHA MGOGORO ULIOUWA YANGA NA KUUNDA PAN
Matatizo ya wanachama kufuata mkumbo na kutokupima mambo wakamsikiliza kocha wa Zaiere, Tambwe Leya na kuwapuuza wachezaji kwa kila jambo ambalo Tambwe aliwaambia,baada ya ile mechi ya kwanza kule Nigeria kutoka sare kocha aliapa kuwa ni lazima wataiondosha katika mashindano Enugu na baada ya kutolewa akashusha lawama nzito kwa wachezaji akina Boi Iddy, Sunday Manara, Omary Kapera, Gibson Sembuli kuwa wameihujumu timu kwa hiyo na kwamba wanachama waamue moja atoke yeye au wachezaji ndipo wachezaji walipotimka kwa kuzingatia kuwa hatukuona kosa lao.
Wakubwa wote wakaenda kuunda timu inayoitwa Nyota Afrika ya Morogoro na wale waliokuwa watoto wakajiunga na Pilsner ya Dar es Salaam na baada ya mwaka akina Sembuli wakarudi kuungana na vijana wao ambao ndio walikuwa sasa moto wa kuotea mbali na kuunda Pan African kwa mashart kuwa wale vijana wote wapewe kazi na kweli wote waliajiriwa kiwanda cha Madawa, hivyo ndivyo ilivyoundwa Pan ikiwa chini ya mzee Tabu Mangara na Shiraz Sherrif.
MATATIZO ALIYOKUMBANA NAYO SAID EL MAAMRY VITUKO NA UKOROFI WA PONDAMALI
Kama kuna watu waliokuwa wakorofi ndani ya uwanja na wapole kabisa tena waungwana nje ya uwanja basi ni Juma Pondamali. Hawa akina Haruna Moshi, Athuman Idd au Juma Kaseja wanasingiziwa tu, lakini kamwe Pondamali hakuachwa timu ya Taifa.
Mwenyekiti wa FAT wakati huo alishamfungia Pondamali mara tano kwa utovu wa nidhamu ikiwa ni hasa kupiga waamuzi ambao walikuwa wanaacha majukumu yao na kutoa maamuzi ambayo yeye kwake aliona si sahihi.
Mechi alizofungiwa ni ile ya Mwanza kati ya Pan na Tumbaku alifungiwa miezi mitatu, Pan na Simba alifungiwa miezi sita pia alifungiwa miaka mitano kwa kuanzisha fujo nzito kati ya Pan na Simba tena mechi zote hizo zilivunjika mapema tu kutokana na fujo za Pondamali lakini adhabu ile alisamehewa na FAT ya El Maamry baada ya kutangaza kuwa anaachana na soka kabisa, haukupita muda pale mjini Songea tena Pan na Majimaji alileta vurugu kubwa lakini mechi iliendelea na yeye kufungiwa mwezi mmoja. Pondamali tena alifanya balaa jingine kubwa mjini Arusha kati ya Pan na Kiltex tena akiwa mchezaji wa akiba baada ya kuingia uwanjani na kumpiga ngwala refa na pambano kuvunjika.
Vituko vya Pondamali vilikuwa ni hatari kuviona bora usimuliwe aliwahi kupewa kadi ya njano baada ya kudaka shuti kali la Mustafa Nagari wa Sudan na kulibana katikati ya miguu na kushika kichwa na mwamuzi alidhani ni bao na baadaye akawaonyesha mashabiki mpira,hizo ni mbwembwe za Pondamali ambazo hakuiga kwa mtu ingawa anasema na Mambosasa naye alikuwa na vitu kama hivyo ingawa si vingi
ANAMSHUKURU SUNDAY KAYUNI
Baada ya kucheza Yanga 1986 hadi 1991 na mwaka 1992 kupandisha Pan tena na kuambiwa mzee alitimkia AFC Leopards ya Kenya alikoitwa na rafiki yake kipenzi Mahamud Abass aliyekuwa Kenya One na kufikia kwanza timu ya Luo Union kama njia tu , na kukipiga pale hadi mwaka 1996 alipoamua kuachana na soka na kuelekea Muheza kuwa mkulima, ndipo kocha maarufu hapa nchini ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni alipomwita na kumlazimisha kuchukua mafunzo ya ukocha mwaka 1997 pale Tandika Mabatini.
"Namshukuru sana Kayuni," anasisitiza Juma Pondamali maarufu kama Mensah, mwenye familia ya watoto wanane ambao ni Kinyanjui, Salama ambaye yuko Uingereza, Masiku, Nassoro, Babby, Fammy ambaye anafuata nyayo zake katika soka, Mensah na Mussa na mkewe ambaye ni raia wa Uingereza
MECHI ISIYOTOKA KICHWANI KWAKE DAIMA
Pondamali anazungumzia kwa hisia kali kuwa mechi ambayo hatoisahau ni ile waliyocheza na Zambia na kuwapeleka Lagos katika fainali za Mataifa ya Afrika. anasema Wazambia walikuwa ni balaa maana kuna wakati nusu saa nzima mpira ulikuwa katika goli la Stars na yeye ilikuwa ni kuokoa tu na kubutua mbele na wenyewe wanaweka chini wanakuja ilikuwa ni balaa, "Mazambia yale yalikuwa yanaongozwa na Godfrey Chitalu, Obby Kapita, Pele Kaimana, Hakimu Musenge ilikuwa ni shughuli pevu."
Pondamali ambaye ni shabiki wa Barcelona na Real Madrid anakumbuka Taifa Stars iliundwa na yeye, Leopard Tasso, Mohammedy Kajole, Leodegar Tenga, Salim Amir, Jella Mtagwa, Omary Hussen, Thueni Ally, Adolf Rishard, Peter Tino, Mohammed Salum na kocha alikuwa kutoka Poland akisaidiwa na Joel Bendera.
WALIVYOPIGANA MATAIFA HURU LAGOS NIGERIA 1980
�Chini ya kocha Mpoland na msaidizi wake Bendera timu iliweka kambi Mexico na moja kwa moja kuelekea Nigeria kupigana katika kundi la kifo na timu zenye wachezaji wengi wa kulipwa kasoro Tanzania, ikiongezewa nguvu na Ahmed Amasha, Juma Mkambi, Mtemi Ramadhani na Mohamedy Bakari Tall, tukiumana na Misri,wenyeji Nigeria na Ivory Coast jambo ambalo hadi leo mwaka wa 29 vijana wameshindwa kufika huko na wala kutoa wachezaji bora kama ilvyokuwa kwa Omary Mahadhi na Maulid Dilunga,� anasema mkongwe huyo.
JE SOKA LIMEMSAIDIAJE
Ana shamba Muheza, Tanga na alijenga nyumba Mburahati, Dar es Salaam na sasa anaishi Kigamboni ambako watoto wake walimnunulia nyumba na kupitia ukocha ana viwanja viwili Bunju, jijini Dar es Salaam ambako atakuwa anaishi baadaye lakini soka limemfanya kujuana na watu wengi.
Huyo ndiye Pondamali aliyezaliwa Dar, kukulia Dar na sasa anazeekea Dar.
Mwandishi wa makala hii ni mchambuzi wa soka na anafanya kazi Bandari anapatikana 0652875794 au Email kennymwaisabula@yahoo.com
source
mwanaspoti
No comments:
Post a Comment