Monday, January 9, 2012
09 JAN . Simba, Azam vita Zanzibar usiku wa leo
LEO ni leo Uwanja wa Amaan mjini hapa wakati Simba na Azam zitakapomenyana kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi.
Simba imeingia hatua hiyo baada ya kushika nafasi ya pili kwenye kundi lake nyuma ya Jamhuri, wakati Azam imeongoza kwenye kundi mbele ya Mafunzo.
Ni mchezo unaokutanisha timu mbili zinazofahamiana vizuri, ambapo zote zinashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara na mara nyingi zinapokutana mchezo huwa wa ushindani mkubwa.
Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall alisema juzi kuwa Simba isitarajie kupata mteremko katika mchezo huo na kuwa amekiandaa vizuri kikosi chake kwa mashindano hayo, hivyo ana imani kitatoa ushindani wa hali ya juu katika mchezo huo.
Hall alisema kuwa kama walivyojiandaa kwa mchezo kati yao na Yanga na kuifunga mabao 3-0 basi, Simba itarajie kupata upinzani mkali kutoka kwa kikosi chao.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic naye amesema vijana wake wapo tayari kwa mchezo huo na ana matumaini watafanya vizuri.
Simba ilifanikiwa kutinga hatua hiyo bada ya juzi kuifunga KMKM mabao 2-0 wakati Azam ilifikia hatua hiyo kwa kuifunga Yanga mabao 3-0 michezo ya mwisho ya makundi.
Mabao ya Simba juzi yalifungwa na Patrick Mafisango na Salum Machaku.
Nusu fainali ya pili inatarajiwa kuchezwa kesho katika uwanja huo kwa kuwakutanisha Mafunzo na Jamhuri zote za Zanzibar.
Simba ndiyo bingwa mtetezi wa mashindano hayo, ambapo ilitwaa kombe hilo mwaka jana kwa kuifunga Yanga mabao 2-0 kwenye fainali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment