Friday, January 6, 2012
06 JAN.YANGA USO KWA USO NA AZAM LEO
LEO ndiyo leo kwenye uwanja wa Amaan wakati Yanga ikiwa na kikosi chake kamili itaivaa Azam, huku Mafunzo ikipepetana na Kikwajuni ili kuamua timu mbili za Kundi B zitakazofuzu kuingia nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi.
Macho na masikio ya wengi yatakuwa majira ya saa 2:00 usiku wakati mabingwa wa Tanzania Bara Yanga watapoivaa Azam FC ikiwa ni wiki chache tangu walipofungwa 2-0 na Azam kwenye mchezo wa kirafiki, lakini kabla ya mchezo huo majira ya saa 10:00 jioni kutakuwa na mechi ya wenyeji, ambapo klabu ya Mafunzo itaivaa vibonde Kikwajuni na kama wakishinda au sare watakuwa wamefuzu kuingia hatua ya pili.
Azam inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne sawa na Mafunzo inayoshika nafasi ya pili wakitofautiana kwa mabao na Yanga inayoshika ya tatu na pointi tatu na Kikwajuni wanaburuza mkia bila ya pointi.
Washindi wawili leo watawasubili wenzao kutoka Kundi A lenye timu za Simba, KMKM, Miembeni na Jamhuri.
Yanga mwanzoni walionyesha kutoyapa umuhimu mashindano hayo na kocha wao Kostadin Papic aliamua kuteua kikosi cha pili na kuwaruhusu wasaidizi wake, Fred Felix Minziro na Aboubakar Salum kuinoa timu hiyo, lakini kocha huyo ameonekana amebadilisha mawazo na leo anatarajiwa kutumia kikosi chake bora.
Papic jana aliingia Zanzibar akiwa na nyota wake wote kuikabili Azam timu inayopewa nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo msimu huu.
Akizungumzia uamuzi wake wa kutumia kikosi cha kwanza badala ya kile cha pili Papic alisema kila kitu kinawezakana kwa sababu mashindano hayo ni sehemu ya maandalizi ya timu hiyo.
''Mechi ya Azam itakuwa ngumu, lakini tunajiandaa kupambana, kati ya timu mbili zitakazofuzu, naamini na sisi tutaingia hatua ya pili, kwa sababu uwezo tunao,'' alisema Papic.
Kocha wa Azam, Stewart Hall amefurahishwa na hatua ya Yanga kutumia kikosi kamili na kusema kuwa sasa anaamini timu yake itacheza soka la uhakika.
“Kama Yanga itashusha kikosi kamili cha timu hiyo itakuwa ni faraja kwetu kwa sababu tutapata ushindi wa jasho kwa sababu tutacheza na timu inayofahamu soka,”alisema Stewart.
Alisema,“Awali nilikuwa na wasiwasi wa kucheza na timu B ya Yanga kwa sababu ushindi wangu usingekuwa wa jasho kwani soka wanalocheza halina tofauti na soka linalochezwa na timu za Zanzibar.”
''Kiujumla kikosi kiko vizuri tayari kwa mchezo huo, isipokuwa waamuzi wawe sawa kwani ndiyo wamekuwa kikwazo kwetu,''alisema Stewart ambaye katika mechi zote mbili za awali amekuwa akikumbwa na mkosi wa kutolewa nje na waamuzi kwa kile kinachodaiwa anavuka mstari wakati wa kuelekeza.
Yanga watashuka dimbani wakitegemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa nyota wao wa zamani, Abdi Kassim na Gaudence Mwaikimba waliojiunga na Azam wakati wa dirisha dogo.
Stewart alisema aliwapumzisha Kipre Tchetche na Jabir Aziz katika mechi yake dhidi ya Mafunzo ili kujiandaa na Yanga leo.
Mabingwa hao wa Tanzania wamepoteza mwelekeo katika kipindi hiki cha maandalizi wakiwa wamepoteza mechi moja na kutoa sare moja huku wakiandamwa na migogoro kati ya viongozi, kocha na wachezaji wao.
Mashabiki wa Yanga wanaamini ushindi kwenye mchezo wa leo na kutwaa ubingwa wa mashindano hayo kutarudisha utulivu ndani ya klabu yao.
Safu ya ushambuliaji ya Yanga itaongozwa na Pius Kisambale akisaidiana na Jerryson Tegete anayesaka kurejesha makali yake mwaka huu.
Wakati huohuo; Timu ya Jamhuri iliamka usingizini na kuichapa KMKM kwa mabao 3-1 kwenye mchezo wa kwanza wa Kundi A.
Karamu hiyo ya Jamhuri ilifunguliwa dakika ya 13 na Ally Juma kabla ya Juma Othman kufunga bao la pili katika dakika ya 26 na msumari wa mwisho ulishindiliwa dakika ya 80 na Seleman Ally na bao la kufutia machozi la KMKM lilipachikwa wavuni na Ame Khamis katika dakika ya 28.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment