Friday, January 6, 2012
06 JAN.MSIKILIZE MZAZI WA MBWANA SAMATA
BABA mzazi wa mshambuliaji Mbwana Samata, Ally Samata ameibuka na SAKATA la timu ya soka ya Kimbangulile kudai timu ya Kimbangulile ndio wenye haki ya kupewa fedha za mauzo ya chipukizi huyo kwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Kauli hiyo ya Mzee Samata imekuja kutokana na maamuzi yaliyotolewa juzi na Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambao ulisema kuwa Kimbangulile imeshindwa kutoa vielelezo kuonesha kuwa iliingia gharama za mazoezi kwa mchezaji husika wakati akiichezea timu hiyo.
Huku kamati hiyo ikidai kuwa kuhusiana na suala asilimia tano ya malipo kwa ajili ya mauzo ya mchezaji huyo ambazo timu hupewa kwa kumlea mchezaji zitalipwa na timu yake mpya itakapokuja kuomba ITC.Baba huyo alisema timu ya Kimbangulile ilimuomba awape Mbwana akiwa na umri wa miaka 11 aliwapa kwa kuingia nao mkataba na walikuwa wakimfanyia kila kitu ikiwemo mavazi na chakula.
"Nashangaa kusikia kwamba Kimbangulile hawana haki ninachokijua mimi niliingia nao mkataba wa kumchukua Mbwana na walifanya kila alichokuwa anakihitaji ikiwemo posho jezi, chakula, viatu na mambo yote muhimu kwa mchezaji," alisema Samata.
Alisema kama kuna haki yao wapewe na atashangaa sana akisikia kuwa wamenyimwa na utakuwa ni uonevu wa hali ya juu kwa kuwa Mbwana mpaka kufika hapo alipo alianzia kwenye timu hiyo.
Kwa upande wake Katibu wa timu ya Kimbangulile Saidi Salehe alisema kuna ulaghai ambao ulifanywa tangu mwanzo na viongozi wa TFF ambao wanauendeleza hadi sasa.Alisema hata mchezaji huyo alipokuwa anachukuliwa na timu ya Mbagala Market kwa sasa Afrikan Lyon kuna kiongozi ambaye alisimamia kufanya ubabaishaji.
"Makamu wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani ndiye ambaye alifanya ujanja wa kumtoa Kimbangulile na kumpeleka Mbagala Market kwa kuwa hatukuwa na fedha ilikuwa ngumu kubishana kwa kuwa walijipanga kwa hilo,"alisema Salehe.Alifafanua kuwa kuna Academy ambayo wanasema ndio ilimlea Mbwana kitu ambacho si kweli.
Alisema wao katika maamuzi yao wanataka risiti za kila kitu sasa watapata wapi risiti ambazo walimnunulia chakula, sabuni na vitu vingine vidogovidogo huku hakuwa peke yake klabuni hapo.
"Tuna ushahidi wa kila aina ikiwemo fomu za kujiunga kwake kwenye mashindano ya Copa Coca Cola akitokea kwenye timu yetu na kushiriki kwenye ligi ya Wilaya ya Temeke Tefa, lakini bado wanasema wanataka ushahidi ushahidi gani,"alihoji Salehe na kuongeza kuwa
"Wanasema tangu mwanzo tulikuwa wapi wakati tumeanza kufuatilia hili suala siku nyingi tangu mwezi wa tatu tukifika Mkurugenzi wa mashindano wa TFF Sadi Kawemba anatuweka hadi jioni bila kutuambia chochote na matokeo yake hutuambia njooni siku fulani ninaweza nikasema katika hili TFF wanahusika moja kwa moja"alisema Salehe.
Aliongeza kuwa kabla ya Kamati kutoa maamuzi hawakutaka kuliweka wazi suala hili kwa kuwa Kawemba aliwakataza kwenda kwenye vyombo vya Habari ndio maana watu wote wanajua wao wameibuka kumbe walikuwa wanafuatilia bila kupewa ushirikiano.
Pamoja na malalamiko hayo msemaji TFF, Boniface Wambura alisema kuwa timu hiyo imekata rufaa kwenye Kamati ya Rufani hivyo Kamati itatengeneza utetezi wake na kuuwasilisha kwenye Kamati ya Rufani itakaposikiliza rufani ya hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment