Sunday, May 13, 2012
13 MAY.Twiga wachapwa nne na Zimbabwe
TIMU ya taifa ya soka ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars kwa ‘bakhti mbaya’ jana imechapwa mabao 4-1 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo ulikuwa ni mahasusi kwa kuzinoa timu hizo zinazojiwinda na mechi zake za kuwania kucheza fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) ambazo Twiga itakwaana na Etthiopia Mei 26 mwaka huu huku Zimbabwe itakipiga na Nigeria.
Kipigo cha Twiga dhidi ya Zimbabwe ni mara ya pili ambapo mara ya kwanza ilikuwa nusu fainali ya Kombe la COSAFA ambapo katika mechi hiyo iliyochezwa Julai 5 jijini Harare, Zimbabwe ilishinda kwa penalti 4-2.
Aidha, timu ambazo jana ilikuwa mara ya tatu kukutana, mara ya pili walikwaa na kwenye michezo ya All Africa Games (AAG) iliyofanyika Maputo, Msumbiji ambapo timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.
Katika mchezo wa jana, Rufaro Machungura aliiandikia Zimbabwe bao la kwanza katika dakika ya 5 ya mchezo baada ya mabeki wa Twiga kujichanganya.
Dakika ya 17 Nokuthula Ndolovu alimalizia kazi nzuri ya washambuliaji wake kwenye eneo la hatari na kuandika bao la la pili ambalo lilidumu hadi timu hizo zinakwenda mapumziko ambapo Zimbabwe ilikuwa ikiongoza mabao 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kucheza kwa taratibu kabla ya Asha Rashid kuiandikia Twiga bao lake pekee katika dakika ya 46 akimalizia kazi nzuri ya Mwanahamis Omari.
Zimbabwe ilitikisa nyavu za Twiga kwa mara ya tatu katika dakika ya 54 kupitia kwa Nokuthula alipotumia vema uzembe wa beki wa Twiga Fatma Khatib aliyekuwa katika harakati za kuokoa krosi yake.
Rufaro Machungura alifunga karamu ya mabao kwa Zimbabwe katika dakika ya 74 ambalo lililidumu hadi dakika 90 ya mchezo huo iliyomalizika kwa Zimbambwe kushinda 4-1.
Aidha, mchezo huo ambao ulichelewa kupigwa kutoka na mvua iliyonyesha leo jijini Dar es Salaam, Mwamuzi wa kimataifa Judith Gamba alimzawadia kadi ya njano nyota wa Twiga Fatma Bashir kwa kumchezea vibaya Rufaro.
Katika mchezo huo Twiga ilifanya mabadiliko na kuwatoa Rukia Khamis, Zena Khamis, Mwajuma Abdallah, na Fatma Hatib na kuwaingiza Fadhila Hamadi, Amina Ally, Siajab Hassan na Mwanaid Tamba.
Baada ya mchezo huo Twiga ambayo ilipata nafasi nyingi za wazi na kushindwa kuzitumia walidai kufungwa kwao kulichangiwa na mvua
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment