tuwasiliane

Friday, May 11, 2012

11 MAY.Ma-DC wengi walioteuliwa na Rais hawana sifa


RAIS Jakaya Kikwete juzi alifanya mabadiliko makubwa ya wakuu wa wilaya nchini, huku akiwatupa nje 31 na kuteua wapya 70 kati ya 133 aliowateua, ikiwa ni wiki moja tu tangu afanye mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri. Katika mabadiliko hayo, Rais amewahamisha wakuu wa wilaya 48 na kubakiza 15 katika vituo vyao vya awali.

Hata hivyo, uteuzi huo umeibua hisia hasi kutoka kwa wananchi kote nchini siyo kutokana na idadi kubwa ya wakuu hao wa wilaya, bali uwezo mdogo wa wengi walioteuliwa kuongoza wilaya hizo wakati huu ambapo nchi inakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi na wananchi wana hali ngumu ya maisha, hivyo kuhitaji watu mahiri kuongoza wilaya hizo ambazo hasa ndizo zinazopaswa kuwa vitovu vya maendeleo.

Sisi hatushangai hata kidogo kuona wananchi wengi wanapinga au kubeza uteuzi wa wengi wa wakuu hao wa wilaya na hatushangai pia kuona wananchi hao wakifanya hivyo kwa hisia kali wakiwa katika mfadhaiko mkubwa. Tunasema hivyo kwa sababu mengi ya matatizo na mateso wanayoyapata wananchi hivi sasa yametokana na uongozi mbovu na dhaifu unaoendelea kuzamisha maendeleo ya nchi yetu na ustawi wa watu wake. Hivyo, wananchi walikuwa na matumaini makubwa kwamba wangeteuliwa watu mahiri, makini, wenye uadilifu, uwezo na uzalendo ili waweze kuondoa uozo uliokithiri katika halmashauri za wilaya.

Tunapenda kutahadharisha hapa kwamba hasira za wananchi kamwe zisichukuliwe kwamba zinahoji mamlaka ya Rais ya kuwateua katika nafasi mbalimbali watu anayeona wanafaa, kwani hakuna ubishi hata kidogo kwamba Katiba inamruhusu kufanya hivyo. Kinachohojiwa na wananchi ni uwezo wa watu aliowateua, ikiwa ni haki yao kikatiba kwani wao ndiyo mamlaka ya juu inayomuweka au kumuondoa rais madarakani.

Katika mazingira ya kidemokrasia, wananchi hawatazamiwi kukaa kimya pale wanapohisi kuna matumizi mabaya ya madaraka. Pia hawategemewi kukaa pasipo kupaza sauti wanapohisi uteuzi wa wakuu hao wa wilaya umeegemea mno katika kutimiza malengo ya kisiasa ya chama fulani badala ya maslahi ya wananchi wote katika mfumo wa siasa za vyama vingi. Hakika hawawezi kutegemewa kufunika kombe eti mwanaharamu apite pale wanapohisi ‘Ofisi ya Mkuu wa Wilaya’ inadhalilishwa kwa kuongozwa na mtu au watu wasio na sifa au wasiofaa.

Wananchi wengi wa kada zote nchi nzima wameghadhabika. Kama habari tuliyochapisha katika gazeti hili leo inavyosema, wananchi jana walionyesha kutoridhishwa na uteuzi wa wakuu wengi wa wilaya, huku wengine wakisema huo ni mpango maalumu wa CCM kujipanga kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kuweka makada wake katika nafasi hizo nyeti. Wengine wanahisi huo ni mradi mahsusi wa kugawana vyeo na kulipana fadhila.

Serikali imesema itawapa wakuu hao wa wilaya mafunzo ya wiki mbili na baadaye watapewa mtihani. Lakini wananchi wanahoji itawezekanaje katika muda huo mfupi wapate ujuzi na uwezo wa kuongoza wasomi walio katika idara mbalimbali za serikali na taasisi za umma wilayani, huku wengine wakisema baadhi ya wakuu hao wa wilaya hawana elimu ya kutosha.

Ni kweli kwamba ukuu wa wilaya ni nafasi nyeti, hasa katika wakati tuliomo wa kufufua uchumi, kuondoa wananchi katika umaskini wa kutisha waliomo na kupambana na ufisadi na rushwa. Hivyo, mbali na uadilifu wananchi wangetegemea wateuliwe watu wenye elimu ya kutosha, wenye rekodi ya utumishi uliotukuka, uzoefu mkubwa katika uongozi na wenye uwezo wa kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo, ikiwamo kilimo, elimu na kadhalika.

Badala ya kupoteza muda na fedha kutoa mafunzo pengine kwa wakuu wa wilaya wasiofundishika, Serikali ingetoa malengo kwa kila mmoja kulingana na mazingira ya wilaya anayokwenda kufanya kazi, lengo kuu likiwa ni kuwaletea wananchi maendeleo badala ya itikadi za kisiasa ambazo kamwe haziwezi kuwapa tija au shibe.

SOURCE.www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment