tuwasiliane

Friday, May 11, 2012

11 MAY.Hujuma, joto vyaitesa Simba Sudan


HUJUMA! Jamani tunahujumiwa huku, hicho ndio kilio cha viongozi na kocha wa Simba, Milovan Cirkovic baada ya kutelekezwa kwa siku nzima kwenye hoteli ya Sharga na wenyeji wao Al Ahly Shandy pamoja na Shirikisho la Soka la Sudan.

Simba iliyofikia kwenye hoteli hiyo iliyopo jijini Khartoum, ilitegemewa kuondoka jana saa nne asubuhi kwa basi kuelekea mji wa Shendi tayari kwa mchezo wao wa marudiano wa Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya wenyeji, Al Ahly hapo Jumapili.

Lakini hadi majira ya saa tisa alasiri si viongozi wa chama cha soka cha Sudan wala viongozi wa timu ya Al Shandy waliofika hotelini hapo kwa ajili ya kuwachukua ili kuwapeleka mjini Shendi kutapofanyika mchezo huo.

"Hii ni hujuma kabisa, tumekwama hapa hotelini kwa siku nzima na bado tuna safari ndefu kwenda huko Shendi," alisema Milovan.

"Kabla ya kuja, walituambia kila kitu kimepangwa, lakini si kweli, hata hivyo tutajitahidi tuwafunge," alisema Cirkovic.
Mwishoni mwa mwezi uliopita chanzo chetu kilizungumza na kipa wa kimataifa wa Tanzania na timu ya Ferroviaro Maputo ya Msumbiji, Mohamed Mwalami aliwatahadharisha viongozi wa Simba juu ya vitendo kama hivyo.

Kipa huyo mkongwe aliitahadharisha Simba kuhusina na hujuma za waarabu hao wawapo kwao kwa kuwataka viongozi wa klabu hiyo kuhakikisha wanailaza timu jijini Khatoum na si Shendi pindi watakapokwenda Sudan kwa ajili ya mchezo wa marudiano.

"Jambo lingine ni kwamba viongozi wa Simba wasikubali timu ilale Shendi itakapokwenda Sudan ni bora walale Khatoum, sisi tulifika saa tisa za usiku, lakini hoteli tumekuja kupata saa sita mchana siku ya pili ambayo ndiyo ya mchezo, ebu angalia jamaa walivyo na fitna mbaya,"alisema Mwalami.

Lakini, Katibu Mkuu wa Simba, Godfrey Nyange Kaburu alisema wao wangetuma mtu mapema huko Sudan ili akawatafutie hoteli na kuandaa mazingira yote kabla ya kuelekea huko. Kitu ambacho hakikufanyika.

Hata hivyo; jana mkuu wa msafara wa timu ya Simba, Hussein Mwamba, ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) alilalamikia hatua hivo kuwa si ya kimichezo.

"Hii itaiathiri timu, kwa sababu tulifika Khartoum saa nane usiku Jumatano, wachezaji walipata muda mchache wa kupumzika tukitegemea timu ingeondoka saa nne asubuhi kwenda huko Shendi, lakini wamezidi kutuchosha hapa," alilalamika Mwamba.

Mwenyekiti wa Simba, Ismael Aden Rage alisema lengo la hujuma hiyo ni kuwachosha wachezaji na kuwanyima muda wa kufanya mazoezi.

"Hii ndio fitina ya soka la Ki-Afrika, lakini limepitwa na wakati", alisema Rage.

JOTO KALI

Kutokana na hali ya joto kuwa kali sana hapa Khartoum, wachezaji walilazimika kukaa mapokezi ya hoteli muda wote kutokana na joto kali nje kuwa zaidi ya nyuzi joto 37.

Kwa muda mwingi, wengi walilazimika kulala katika viti vilivyopo sehemu ya mapokezi baada ya muda wa kuendelea kushikiria vyumba kupita kwa mategemeo kuwa timu ingeondoka hotelini saa nne asubuhi kama ilivyopangwa.

Kutokana na joto kali, Rage alilazimika kwenda mtaani kununua vinywaji na vyakula ili wachezaji wapozee njaa wakati wakisubiri chakula ambacho aliagiza kipikwe kwa ajili ya wachezaji.

"Kutokana na joto kali, wachezaji inabidi wale vyakula na vitu vya majimaji kwa wingi ili kuongeza nguvu mwilini kutokana na kupoteza maji mwilini kwa joto", alisema Rage.

"Pamoja na hujuma hizi, tulikwisha waandaa wachezaji kisaikolojia kuwa wategemee njama kama hizo kutoka kwa timu za Sudan," alisema Rage.

Timu ya Simba inapanga kulalamika kwa kamishna wa mechi kwa kitendo cha kutelekezwa hotelini kwa muda wa saa zaidi ya kumi.

No comments:

Post a Comment