Wednesday, May 9, 2012
09 MAY.BAADA YA KUTIMLIWA NA JK MKULO, MAIGE KORTINI
MARA baada ya Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa wiki iliyopita kulisuka upya baraza lake la mawaziri kwa kuwatosa mawaziri sita kati ya wanane waliokuwa wametajwa kwa kashfa mbalimbali katika ripoti ya Mdhibiti Mkuu na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), mawaziri wawili wamo mbioni kushitakiwa kortini.
Habari kutoka ndani ya serikali zinasema tayari maofisa wa serikali wanaandaa makabrasha ya kuwafikisha mahakamani maofisa kadhaa akiwemo aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige na aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo.
MUSTAFA MKULO
Mkulo ndiye aliyekuwa waziri wa kwanza kutakiwa na wabunge ajiuzulu kwa kutuhumiwa kuvunja Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) ili kuficha tuhuma zake ikiwamo uuzaji wa kiwanja Na.10 kwa Kampuni ya Mohamed Enterprises (MeTL).
Ukaguzi wa CAG ulibaini kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina na Wizara ya Fedha zilihusika moja kwa moja katika uuzwaji wa kiwanja hicho Na.10 kilichopo kando ya Barabara ya Nyerere bila kuishirikisha bodi ya CHC.
Aidha, CAG alibaini kuwapo kwa matatizo katika hati ya madai ya Shilingi bilioni 2.4 kutoka katika Kampuni ya DRTC kama gharama za ulinzi na tozo la matumizi ya barabara ya kuingilia kwenye Kiwanja Na.192 kando ya Barabara ya Nyerere.
Upungufu pia ulionekana kwenye uuzwaji wa jengo la Kampuni ya Tanzania Motors (TMC) lililopo kiwanja Na.24 kilichopo katika eneo la viwanda la Chang’ombe kwa Kampuni ya Maungu Seed.
EZEKIEL MAIGE
Maige akiwa Waziri wa Maliasili na Utalii ripoti ya CAG ilieleza kuwa ofisi yake ilipoteza Shilingi 874,853,564 baada ya kufanya uamuzi wa upendeleo wa kutoa kiwango cha chini cha mrahaba kwa mauzo ya misitu.
Katika kipindi cha ukaguzi wa hesabu za Shirika la Hifadhi ya Taifa Tanzania (Tanapa) ilibainika kuwa shirika liliingia katika mkataba na Kampuni ya CATS Tanzania LTD unaohusiana na matengenezo ya kawaida, ufungaji wa vifaa vya mawasiliano na vifaa vingine katika mkataba wa jumla ya dola milioni moja za Marekani.
Alishutumiwa kwa kutengeneza mazingira ya rushwa katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji, ugawaji ambao inadaiwa ulitawaliwa na dosari nyingi ikiwa ni pamoja na kutangaza majina ya waliopata vitalu bila kuonyesha ni vitalu vipi walivyopewa. Aidha, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi na Maliasili ilieleza kuwa kampuni 16 zilizopewa vitalu hivyo hazikuomba na kwamba vitalu hivyo vilikuwa vya daraja la kwanza na la pili.
Mbali na tuhuma hizo, Maige hivi karibuni alidaiwa kununua nyumba kwa Dola za Marekani 700,000 iliyopo Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, tuhuma ambazo alizipinga na kusema kuwa nyumba hiyo ameinunua kwa Dola 410,000, (sawa na zaidi ya shilingi milioni 600 za Kitanzania).
Habari za ndani kutoka serikalini zilizotufikia zinasema mara baada ya Rais Kikwete kutoa tamko la wahusika wa ubadhirifu huo ‘washughulikiwe’, tayari nyaraka mbalimbali zimeanza kushughulikiwa na vyombo vya dola ili kuona nani aliiba na nani hahusiki. Waliokuwa mawaziri na kutemwa nao wanamulikwa na vyombo vya sheria.
WOTE KUSHITAKIWA
Mwenyekiti wa Democratic Party, (DP), Christopher Mtikila amesema hivi sasa anaandaa mashitaka kwa mawaziri wote wanane walioonekana na Bunge kuliingiza taifa katika hasara kubwa.
“Mbona Amatus Liyumba aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania alishitakiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi, hawa wote tutawashitaki, tuache tabia ya kipumbavu ya kupendeleana,” alisema Mtikila jana alipoongea na mwandishi wetu.
SOURCE GLOBAL PUBLISHERZ
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment