Sunday, January 8, 2012
08 JAN. Kiwango kibovu Yanga chamchefua Papic
KOCHA Mkuu wa Yanga, Konstadin Papic amesema hakuridhishwa na kiwango kibovu kilichooneshwa na wachezaji wake katika mechi ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Azam iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan juzi usiku.
Katika mechi hiyo, Yanga ilifungwa mabao 3-0 na kuaga michuano hiyo.
Akizungumza mjini hapa jana, Papic alisema kuwa mbali ya wachezaji hao kuonesha kiwango cha chini lakini waliweza kuchanganyikiwa baada ya Azam FC kupewa penati katika dakika za mwanzo za mchezo huo.
“Kiwango chao sikuridhika nacho lakini bao la kwanza liliwaathiri wachezaji wangu”, alisema.
Matokeo hayo yaliiwezesha Azam kutinga hatua ya nusu fainali za michuano hiyo huku Yanga ikifungasha virago baada ya kumaliza mechi zake za makundi ikiwa na pointi 3.
Katika mchezo huo, Yanga walionekana kuzidiwa kwa kila idara kutokana na kiwango dhaifu walichoendelea kukionesha tangu kuanza kwa michuano hiyo.
Azam FC ambayo ilionekana kuukamia mchezo huo iliandika bao la kwanza kwa mkwaju wa penati lililofungwa na John Boko katika dakika ya tano baada ya Mohammed Mbegu kumchezea vibaya mshambuliaji wa Azam FC.
Kipre Tchetche ndiye aliyekuwa mwiba mchungu kwa Yanga baada ya kufunga mabao mawili katika dakika ya 29.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Waamuzi Wilaya ya Mjini imemsimamisha mwamuzi Ramadhan Ibada Kibo kuchezesha mashindano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kubainika kuwa alishindwa kumudu kuchezesha mechi kati ya Yanga na Azam.
Katika mechi hiyo iliyochezwa juzi usiku kwenye Uwanja wa Amaan, Yanga ilijikuta ikishindwa kufurukuta tena mbele ya Azam kwa kukubali kichapo cha mabao 3-0.
Kibo ambaye alikuwa mwamuzi wa kati katika mchezo huo alilalamikiwa na baadhi ya mashabiki na viongozi wa Yanga waliokuwepo uwanjani hapo wakimtuhumu kuelemea upande mmoja.
Katibu wa Kamati hiyo, Ramadhan Nassor jana alithibitisha kuwa kamati yake imetoa adhabu hiyo baada ya kukaa na kujadili mchezo huo ambapo imegundua haukuchezeshwa vizuri.
“Kamati ya Wilaya ya Mjini imekaa na kuujadili mchezo wa Yanga na Azam FC na kuamua kumsimamisha mwamuzi Kibo kuchezesha mashindano haya kutokana na kutochezesha vizuri mchezo huo”, alisema.
Aidha kamati hiyo pia imetoa onyo kwa waamuzi wasaidizi Ali Juma Kombo na Mohammed Kassim. Hata hivyo, alisema kuwa kamati hiyo inatarajiwa kukaa tena kulijadili suala hilo.
Yanga ilitarajiwa kuondoka jana kwa boti ya asubuhi kuelekea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea na mazoezi kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara pamoja na michuano ya kimataifa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment