Saturday, January 7, 2012
07 JAN.TP MAZEMBE YAMUONDOA SAMATA CAF
HATIMA ya mshambuliaji Mbwana Samatta kuichezea TP Mazembe ya DR Congo katika michuano ya kimataifa ipo hatarini kutokana na baadhi ya mambo juu ya usajili wake kutokamilika.
Hali hiyo inafuatia baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutangaza kuwa Mazembe haijakamilisha mchakato wa kupata kibali cha Uhamisho wa Kimataifa (ITC), kutokana na hali hiyo kuna uwezekano wa Samatta kutoichezea klabu hiyo katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika inayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Africa (Caf), msimu huu.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura amesema suala la Samatta kucheza au kutocheza linautata kwa kuwa awali Mazembe waliomba ITC ya mchezaji huyo lakini wao waligoma kuwapa kwa kuwa walikuwa hawajamalizana na Simba, lakini baada ya kumalizana, hawakurejea kumalizia mchakato wa kupata ITC hiyo.
“Muda wa kuwasilisha majina Caf umeshapita, mwisho ilikuwa ni Desemba 31, mwaka jana. Samatta anachezaje kama hana ITC? Hilo siyo suala la TFF ila linaihusu Shirikisho la Soka la Congo, japokuwa Caf kuna wakati huwa inatoa muda zaidi wa kupitia majina na kuna kifungu kinachoruhusu mchezaji kucheza hata kama hajakamilisha ITC japo inategemea na mashindano.
“Unakumbuka kilichowatokea Mazembe mwaka jana, walitolewa licha ya yule mchezaji (Janvier Besala Bokungu) kuwa raia wa Congo lakini hakuwa na ITC baada ya kutoka kucheza soka Tunisia na kurejea Congo.
“ITC inatolewa bure na haina malipo ndiyo maana kuna sheria kuwa kama ikichelewa au kukiwa na uzembe, Caf au Fifa wanaitoa wao,” alisema Wambura .
Mazembe imepangwa kukipiga na mshindi kati ya Japan Actual ya Madagascar au Power Dynamos ya Zambia katika mzunguko wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Samatta alisajiliwa na Mazembe, mwaka jana na amekua akicheza katika mechi za Ligi Kuu ya DR Congo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment