tuwasiliane

Saturday, January 7, 2012

07 JAN. Waliomlea Samatta wakwama TFF


KAMATI ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) imesema timu ya Kimbangulile imeshindwa kutoa vielelezo kuhusiana na mchezaji
Mbwana Samatta.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura imeeleza kuwa Kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Alex Mgongolwa ilikutana Desemba 30 mwaka jana kupitia masuala mbalimbali yaliyowasilishwa mbele yake ikiwemo taarifa ya uamuzi wa timu ya Kimbangulile kukata rufani Kamati ya Rufani kupinga uamuzi wake juu ya mchezaji Mbwana Samatta.

“Ikumbukwe kuwa Kimbangulile iliwasilisha malalamiko TFF ikieleza kuwa inastahili malipo
baada ya Simba kumuuza Samatta kwa timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

“Kimbangulile ilitaka ilipwe fidia ya mazoezi (training compensation) na mchango maalumu (solidarity contribution) kwa mujibu wa Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

“Uamuzi wa Kamati ya Mgongolwa ulikuwa Kimbangulile imeshindwa kutoa vielelezo
kuonesha kuwa iliingia gharama za mazoezi kwa mchezaji husika wakati akiichezea timu hiyo.

“Kwa upande wa solidarity contribution ambayo ni asilimia 5 ya mauzo ya mchezaji huyo TP
Mazembe, fedha hizo zinatakiwa kulipwa na klabu yake hiyo mpya ambayo TFF itaitaka kufanya hivyo wakati Samata atakapoombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).

“Hivyo Kamati itatengeneza utetezi wake na kuuwasilisha kwenye Kamati ya Rufani itakaposikiliza rufani ya Kimbangulile,” alisema Wambura.

No comments:

Post a Comment