tuwasiliane

Saturday, January 7, 2012

07 JAN. Chalz Baba ajiengua Twanga Pepeta


MWANAMUZIKI Charles Gabriel ‘Chalz Baba’ ameamua kuachana na bendi ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta na kufanya kazi zake za kimuziki mwenyewe.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwanamuziki huyo alisema ameamua kuachana na bendi hiyo baada ya kuitumikia kwa kipindi cha miaka sita bila mkataba wa kueleweka.

Chalz Baba alisema alijiunga na bendi hiyo tangu mwaka 2005 kwa mkataba wa mwaka mmoja na mara baada ya mkataba wake kuisha hakuongezwa mkataba mwingine hali inayomfanya aone kuna umuhimu wa kufanya kazi zake binafsi.

“Nilikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na Twanga Pepeta lakini baada ya kumalizika nimekuwa nikifanya kazi kama mtoto wa nyumbani,”alisema Chalz Baba.

Katika kujipanga upya mwanamuziki huyo amemteua Benard Msekwa kama meneja wake na
kwamba bendi yoyote itakayotaka kufanya kazi naye lazima iwasiliane na meneja huyo.

Alisema ameamua kufanya kazi chini ya Meneja huyo ili kuratibu shughuli zake za muziki kitaalamu ikiwa ni pamoja na kusimamia kwa haki zake kama mwanamuziki pindi atakaposaini mkataba wa kazi zake za kimuziki.

Alisema kipindi hiki ambacho anafanya kazi kama mwanamuziki binafsi yuko mbioni kutoa albamu yake yenye nyimbo 8 huku nyimbo nne tayari zikiwa zimerekodiwa.

Alizitaja nyimbo hizo kuwa ni Nusu Chizi, Blandina, Baba Fred na Naelekea Wapi ambapo alisema jina la albamu itakayobeba nyimbo litajulikana mara baada ya kukamilisha kurekodi nyimbo zote nane

No comments:

Post a Comment