tuwasiliane

Thursday, December 8, 2011

08 DEC. Mechi ya Simba, Kotoko yaiva


TIMU ya soka ya Asante Kotoko ya Ghana inatarajiwa kuwasili nchini kesho kwa ajili ya mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya Simba utakaofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa.

Mchezo huo ni sehemu ya kukamilisha maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa
Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa wa kampuni ya Future Century Limited, Albert Albano alisema maandalizi yote kwa ajili ya mechi hiyo yamekamilika.

Alisema kuwa timu hiyo itafikia Zanzibar na baadaye kuja jijini Dar es Salaam kwenye hoteli ya Lamada tayari kwa mchezo huo ambao umedhaminiwa na PPF, Kenya Airways, Vanedrick Tanzania Limited, Lamada Hotel na Vanne Fashion Tabata.

“Msafara wa Kotoko utakuwa na watu 40 ambapo utakuwa na waandishi wa habari 10 kutoka
nchini humo”.

Alisema mchezo huo utakuwa wa timu moja badala ya kombaini ya Simba na Yanga kama ilivyotangazwa awali baada ya Yanga kujitoa.

Alisema wao wamekuwa wakipata taarifa kupitia vyombo vya habari kuwa Yanga
hawatashiriki, lakini hata walivyotaka kupata ufafanuzi kutoka kwa viongozi wa Yanga wameshindwa kutokana na kutopokea simu zao.

Albeno alisema bado wanaendelea kuwasiliana nao ili wajue hivyo wamewapelekea barua ya
kutaka kujua nini hatima yao kwa kuwa katika mazungumzo yao kuna makubaliano ya kiofisi ambayo yalifanyika.

"Sisi bado tunaendelea kuwasikiliza Yanga nini watasema maana wamekaa kimya hata simu zetu hawapokei ndiyo maana tumeamua kuitangaza Simba pekee ndiyo inayocheza na Kotoko," alisema Albano.

Alisema katika mchezo huo viingilio vitakuwa Sh 30,000 kwa VIP A, VIP B Sh 15,000 VIP C Sh 10,000.

Kwa upande wa jukwaa la rangi ya chungwa ni Sh 5,000, kijani na bluu ni Sh 3,000.

No comments:

Post a Comment