tuwasiliane

Saturday, October 20, 2012

SAMATTA, ULIMWENGU KUIBEBA MAZEMBE LEO TUNISIA?

TOUT Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) leo ina mtihani mgumu mbele ya Esperance ya Tunisia katika mchezo wa marudiano wa Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mjini Tunis.
Hiyo inatokana na Mazembe kulazimishwa sare ya bila kufungana na mabingwa hao wa Afrika, katika mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Stade du TP Mazembe mjini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wiki mbili zilizopita.
Sare yoyote ya mabao inaweza kuivusha Mazembe hadi fainali, lakini Esperance inapewa nafasi kubwa ya kushinda kwa kuwa itakuwa ikicheza nyumbani.
Mchezo huo tayari umekuwa gumzo kubwa, kutokana na upinzani mkubwa baina ya timu hiyo na hasa baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kubadilisha refa wa mechi hiyo siku tatu kabla ya timu hizo kurudiana.
CAF imeteua marefa wapya wa kuchezesha mechi hiyo ya leo kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Mazembe dhidi ya refa Bakary Gassama kutoka Gambia na sasa Badara Diatta wa Senegal ndiye ambaye sasa atachezesha mechi hiyo mjini Tunis.
Magazeti nchini Tunisia yamepinga uteuzi wa refa mpya kwa sababu anatoka nchi moja na kocha wa Mazembe, Lamine N’Diaye, ambaye ni Msenegal pia.
Mazembe ina washambuliaji hatari wa Kitanzania, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu ambao wote kwa sasa ni tegemeo la timu hiyo.
Katika mchezo wa leo, Mazembe itamkosa beki wake tegemeo, Stopila Sunzu aliyepewa kadi ya pili ya njano (nyekundu) dakika ya pili ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za kawaida kwenye mechi ya kwanza.
Awali, Sunzu kaka wa mshambuliaji wa Simba, Felix Sunzu, alionyeshwa kadi ya kwanza ya njano dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Washambuliaji wote wawili wa Kitanzania walicheza mechi hiyo, Mbwana Ally Samatta alicheza hadi dakika 83 alipompisha Sinkala, wakati Thomas Emanuel Ulimwengu alitokea benchi dakika ya 58 kwenda kuchukua nafasi ya D. Kanda.
Nusu Fainali nyingine ya michuano hiyo inatarajiwa kuchezwa kesho kati ya mabingwa mara sita Afrika, Al Ahly ya Misri na Sunshine Stars ya Nigeria mjini Cairo. Katika mechi ya kwanza ya iliyopigwa huko Ijebu-Ode kwenye Uwanja wa kimataifa wa Dipo Dina, timu hizo zilitoka sare ya kufungana mabao 3-3.
Nahodha wa Sunshine, Godfrey Oboabona aliikosa mechi hiyo baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano katika mechi ya mwisho ya makundi dhidi ya Esperance ya Tunisia, wakati Mohamed Aboutrika alikuwa anatumikia adhabu ya kufungiwa miezi miwili na Ahly. 
Ahly ilipata bao la kwanza dakika ya 18 kupitia kwa Mohamed Nagy, aliyefumua shuti kutoka nje ya boksi na kumtungua Moses Ocheje, kabla ya Mahdy El Sayed kuifungia bao la pili timu hiyo dakika ya 30, wakati Sunshine ilipata bao la kwanza dakika ya 40, kupitia kwa kiungo Mcameroon, Tamen Medrano aliyemtungua kwa shuti la mbali kipa wa Ahly, Sherif Elkramy. 
Wenyeji walisawazisha dakika ya 73 kwa mkwaju wa penalti wa Dele Olorundare baada ya Ajani Ibrahim kuangushwa kwenye eneo la hatari na Mohamed Nagy.
Pamoja na hayo, Mashetani Wekundu wa Cairo walipata bao lililoelekea kuwa la ushindi, dakika moja badaaye kupitia kwa kijana mwenye umri wa miaka 25, Nagy ambalo lilikuwa bao lake la pili kwenye mechi hiyo. 
Beki wa Sunshine, Precious Osasco aliisawazishia timu yake dakika ya 83 kwa shuti la mpira wa adhabu lililomshinda kipa Elkramy.  Nagy alipata nafasi ya kukamilisha hat-trick dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho, lakini kichwa chake kiliupaisha mpira alipokuwa anaunganisha kona.

No comments:

Post a Comment