tuwasiliane

Wednesday, May 9, 2012

09 MARCH.Mbunge Nassari ajisalimisha Polisi


MBUNGE wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, amejisalimisha katika kituo kikuu cha Polisi mjini Arusha, akitii amri ya Polisi iliyomtaka afanye hivyo vinginevyo adhalilishwe.

Hata hivyo, kabla ya kujisalimisha jana alasiri, Nassari aliwasili katika kituo hicho asubuhi na kudai kutokuwa na taarifa rasmi za kutafutwa na Polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Nassari alidai kuwa hakuna mtu aliyemtumia ujumbe kuwa anatafutwa.

Nassari (Chadema) alisema ujumbe alioupata ni wa simu kutoka kwa Ofisa Upelelezi wa Wilaya Faustin Mafwele, ukimpa taarifa kuhusu Kamanda Thobias Andengenye, kuhamishwa na aliombwa kwenda kituoni hapo kuagana naye.

“Sijapata taarifa nyingine ya mimi kuitwa na Polisi na ndiyo maana sasa niko hapa, lakini nimeambiwa wahusika hawapo nirudi saa nane mchana,” alisema asubuhi.

Juzi Naibu Kamishna wa Polisi nchini, Isaya Mngulu alisema yeye binafsi alimtumia ujumbe wa simu Nassari kuhusu kutakiwa Polisi kwa mahojiano.

Mbali na kumtaka Nassari ajisalimishe, pia Polisi ilikuwa ikiwashikilia na kuwahoji viongozi watatu wa juu wa Chadema, kwa kutoa lugha za uchochezi, ubaguzi na ukabila dhidi ya Rais Jakaya Kikwete na wananchi.

Jeshi hilo lilimpa hadi saa 12 jioni juzi mbunge huyo awe amejisalimisha vinginevyo adhalilishwe kwa kumsaka kokote aliko na kumtia ndani, kwani hayuko juu ya sheria ya nchi.

Hata hivyo, taarifa ya Nassari inakinzana na ya Kamishna Mngulu, kwani alisema hakuna mtu ayatembea na ofisi, hivyo Nassari alipaswa kusubiri hapo mpaka viongozi wa juu wa Polisi Arusha warudi.

“Hata kama mimi nimeondoka, wengine si wapo kwa nini hakusubiri hapa nini kinamfanya aondoke?” Alihoji Mngulu.

Viongozi wengine waliohojiwa na kuachiwa kwa dhamana juzi ni pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa (Bavita), John Heche; Diwani wa zamani wa CCM Sombetini ambaye hivi karibuni alihamia Chadema, Alphonce Mawazo na Mwenyekiti wa zamani wa UVCCM Wilaya ya Arusha, Ally Bananga ambaye pia amejiunga Chadema.

Alisema, miongoni mwa matamshi anayotuhumiwa kuyasema Nassari ni kumpiga marufuku Mkuu wa Nchi kukanyaga Arumeru na Kanda ya Ziwa, eti kwa kuwa maeneo hayo ni ya Chadema na wakati wowote watatangaza Rais wao kama ilivyokuwa Sudani Kusini.

Mengine ni kumhusisha mtoto wa Rais Kikwete, Ridhiwani na masuala ya uteuzi wa viongozi wa nchi unaofanywa na baba yake. Alisema hayo matamshi hayana maana yoyote kwa jamii, kwani yana lengo la uchochezi kwa Rais na wananchi wake.

Baada ya kutoa matashi hayo jukwaani, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisimama na kusema kuwa matamshi hayo si ya Chadema bali ni ya vijana hao wenye damu ya moto wa gesi na ni kauli zao binafsi na yeye haziungi mkono.
SOURCE HABARI LEO

No comments:

Post a Comment