
Timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes wameanza vyema kampeni ya kusaka nafasi ya kushiriki kombe la mataifa Africa kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 20, baada ya kuwachapa Sudan goli 3-1.
Katika mchezo huo uliochezwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Ngorongoro Heroes walianza kusheherekea goli la kwanza katika dakika ya 15 lililofungwa na mshambuliaji wa TP Mazembe ya DR Congo, Thomas Ulimwengu ambaye hakumaliza mchezo baada ya kuumia katika kipindi cha kwanza.
Goli la pili lilifungwa katika dakika 20 na chipukizi wa Simba SC, Ramadhan Singano 'Messi' na kupelekea Ngorongoro Heroes kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa goli 2-0.
Ngorongoro Heroes waliandika goli la 3 katika dakika ya 65 kupitia kwa mshambuliaji Saimon Msuva anayekipiga Moro United kwa mkopo akitokea kwenye kikosi cha Azam Academy.
Sudan walipata goli lao la kufutia machozi katika dakika za lala salama kupitia kwa Sharafeldin Shaiboub, na kupelekea mchezo kumalizika kwa Ngorongoro Heroes kushinda goli 3-1.
Kwa matokeo hayo yanaiweka katika nafasi nzuri Ngorongoro katika mchezo wa marejeano utakao chezwa Sudan kati ya mei 4-6 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment