tuwasiliane

Saturday, April 21, 2012

21 APR.Ngorongoro Heroes; kazi ni kazi tu leo


TIMU ya soka ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’ leo inachuana na Sudan katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika kwa vijana wa umri huo.

Mchezo huo unaotarajiwa kuanza alasiri Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa wa vuta
nikuvute huku Kocha Poulsen anayeinoa Ngorongoro Heroes akiahidi kikosi chake kufanya
vizuri kwenye mechi hiyo na kuwapa raha mashabiki.

Akizungumza jana, Poulsen alisema timu yake imejiandaa vizuri kwa mechi hiyo na kiu yao ni
kushinda na hakuna sababu ya kuwa na hofu ingawa katika soka lolote linaweza kutokea.

“Tumejiandaa vizuri, vijana wana ari kubwa ya mchezo, hivyo hatuna hofu, tunaamini mashabiki watafurahi. Nawaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kutushangilia,” alisema Poulsen.

Kwa upande wake Kocha wa Sudan, Azhari Osman El Tahir alisema ingawa haifahamu vizuri timu ya Tanzania, lakini wamejiandaa kushinda kwani kwa muda mrefu walikuwa hawajashiriki mashindano ya vijana ya kimataifa.

Katika mchezo huo viingilio vimepangwa kuwa Sh 3,000, Sh 5,000, Sh 10,000 na Sh 15,000.
Sudan iliwasili nchini juzi ikiwa na kikosi cha wachezaji 20, viongozi kumi na mwandishi wa
habari mmoja kwa ajili ya mechi hiyo ya kwanza kabla ya timu hizo kurudiana jijini Khartoum kati ya Mei 4, 5 na 6 mwaka huu.

Mechi hiyo itachezeshwa na mwamuzi Brian Miiro atakayesaidiwa na Mark Ssonko, Lee
Patabali na Denis Batte wote kutoka Uganda. Ejigu Ashenafi wa Ethiopia ndiye atakayekuwa
Kamishna wa mechi hiyo namba 15.

Fainali za Afrika kwa michuano hiyo zitafanyika Machi mwakani nchini Algeria wakati za Dunia
zitafanyika nchini Uturuki kuanzia Juni hadi Julai mwakani. Katika fainali za Dunia, Afrika itawakilishwa na timu nne za kwanza kwenye fainali za Algeria.

No comments:

Post a Comment