
Mabingwa wa Tanzania Bara na Afrika mashariki na kati, Yanga hawaja afiki maamuzi ya kamati ya ligi ya shirikisho la soka TFF kwa kuwanyanganya point 3 na kuwapa ushindi wa goli 3 na point 3 Coastal Union ya Tanga.
Kamati hiyo ilifikia uwamuzi huo juzi baada ya Yanga kumtumia kimakosa beki wao tegemeo Nadir Haroub Ally 'Canavaro' katika mchezo dhidi ya Coastal uliochezwa machi 31.
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, alisema hawajapata taarifa rasmi, lakini hawawezi kukubali kwa vile Kamati ya Ligi ya TFF haina mamlaka ya kusikiliza rufani.
Alisema kulingana na kanuni ya 25 ya ligi hiyo, rufaa zote zinazohusiana na Ligi Kuu zitasikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF.
“Iwapo mrufani au mrufaniwa hataridhika na maamuzi ya kamati ya Nidhamu, atakata rufaa kwa Kamati ya rufaa ya TFF. Kamati za nidhamu na rufaa zitasikiliza rufaa zote zinazohusu mashindano haya na ufundi,” alisema Nchunga na kuongeza kuwa kutokana na hali hiyo wanasubiri barua ili kuona uamuzi gani watauchukua kuhusiana na jambo hilo.
Hata hivyo, alisema uamuzi wa Kamati ya Ligi ni uonevu kwa Yanga kwa nia ya kuibeba timu fulani na kwamba kwa namna hiyo soka la Tanzania haliwezi kuendelea kwa sababu yanafanyika uamuzi wa manufaa ya timu fulani.
“Ndiyo sababu hizi kamati zinatakiwa ziwe na viongozi wa juu ambao ni wanasheria ili kuepusha mambo ambayo yanaweza kuleta mgogoro kama haya, lakini kwa vile kuna timu fulani zinanufaika ndiyo sababu Yanga inaonewa,” alisema Nchunga.
Lakini akizungumza baadaye jana, mjumbe mmoja wa Kamati ya Ligi, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema Coastal Union haikukata rufani, ila ilicheza mechi na Yanga ikiwa na pingamizi kuhusiana na Cannavaro.
“Pia Kamati ya Ligi huwa haisubiri rufani, yenyewe inafanyia kazi ripoti za mechi na ni sehemu ya utendaji wake, viongozi wa Yanga wanafahamu hilo. Pia ndani ya kamati wapo watu ambao ni wanasheria,” alisema.
Kutokana na kupokwa pointi hizo, mbio za Yanga katika kutetea ubingwa zimeingia kwikwi kwani sasa imepitwa pointi saba na vinara Simba na pointi nne na Azam.
Hata hivyo, Yanga ipo nyuma mchezo mmoja, ambapo kama itashinda kiporo hicho itakuwa imepitwa pointi nne na Simba na pointi moja na Azam
No comments:
Post a Comment