
KOCHA wa Yanga, Kostadin Papic amekemea uzembe wa washambuliaji wake na kudai makosa yao yanaiweka timu hiyo kwenye wakati mgumu.Papic aliyasema hayo wakati wa mazoezi ya jana asubuhi kwenye viwanja vilivyopo katika shule ya Sekondari ya Loyola.
Katika kile kinachoonekana kuchoshwa na tabia hiyo ya washambuliaji kushindwa kufunga, Papic alisisitiza kwamba anataka umakini wa kufunga kutoka kwa wachezaji hao.
Mchezaji mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa siku mbili hizi kocha amekuwa mkali kwa washambuliaji kwa madai kuwa wanamuangusha mara zote hasa wakiwa wanakabiliwa na mechi muhimu.
"Kocha amekuwa mkali sana kwa washambuliaji akidai kuwa hata timu ikicheza vizuri sehemu nyingine zote washambuliaji wasipofunga ni kazi bure,"alisema mchezaji huyo.
Baada ya mazoezi hayo kocha Papic alisema kuwa nia ya mchezo wowote ni ushindi hata kama utacheza vizuri vipi usiposhinda utabaki kuwa wa mwisho.Alisema ili timu ifanye vizuri na iweze kusonga mbele ni lazima iwe na washambuliaji makini na wenye uwezo wa kufunga kila nafasi inapojitokeza.
"Kwenye kila mchezo ushindi lazima hivyo ni lazima washambuliaji wajue namna ya kuzitumia nafasi hizo zinazopatikana," alisema Papic.
No comments:
Post a Comment