tuwasiliane

Wednesday, January 25, 2012

25 JAN. Simba, Coastal mambo hadharani leo


VINARA wa Ligi Kuu Bara, Simba leo wanashuka dimbani kuzindua ngwe ya lala salama ya ligi hiyo, huku wakitarajia kutumia vizuri mwanya wa wapinzani wao Yanga kushindwa kuwashusha kileleni mwa msimamo pale wakatapokuwa wenyeji wa Coast Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga ilikuwa na fursa nzuri ya kuishusha Simba kileleni mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini ilishindwa kufanya hivyo kufuatia kubanwa na sare ya 2-2 dhidi ya Moro United katika siku ya kwanza ya mwanzo wa mzunguko wa pili.

Zote sasa zina pointi 28, lakini Yanga ikibaki nafasi yake ya pili kutokana tofauti ya mahesabu ya mabao ya kufunga na kufungwa kuwapa faida zaidi wapinzani wao, ambao pia wako nyuma kwa mchezo mmoja mpaka leo.

Wekundu wa Msimbazi watasaka pointi tatu dhidi ya Coastal katika hali ya kujiamini yenye kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0 walioupata kwenye mechi ya kwanza mwaka jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Lakini pengine hilo halitatosha kuwapa matumaini sana Simba, hasa ukizingatia kuwa karibu timu zote za Ligi Kuu zilifanya marekebisho ya usajili wakati wa dirisha dogo Januari hii.

Katika usajili wao, Coastal Unionn waliomaliza mzunguko wa kwanza na ushindi wa mechi tatu kati ya 13, imemuongeza kiungo wa zamani wa Simba na Yanga, Edwin Mukenya.

Ni wazi mechi hiyo itakuwa ngumu kwa vile vijana hao wa Tanga hawatapenda kuwa ngazi kwa Simba, lakini pia ushindi kwao itakuwa faraja ya ukombozi wa kujinasua toka kwenye mstari wa kushuka daraja.

Wakati Wagosi wakijipanga hivyo, wapinzani wao leo watashuka dimbani bila kuwa na nyota wawili tegemeo akiwemo wa bei mbaya, Felix Sunzu na winga Ulimboka Mwakingwe ambao wote ni majeruhi.

Kwa maana hiyo, Kocha Milovan Cirkovic atalazimika kumtumia chipukizi Ramadhan Singano ili acheze na mshambuliaji Gervais Gargo, huku wakisaidiwa na viungo Uhuru Seleman na Haruna Moshi'Boban'.

Mbali ya kipute hicho, utamu mwingine wa msuguano wa mzunguko wa pili utakuwa nje kidogo ya jiji, wakati wenyeji na mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC watakapokuwa wakisaka pointi kwenye Uwanja wa Chamazi dhidi ya African Lyon.

Azam katika nafasi ya nne ya msimamo ikiwa na pointi 23, tano nyuma ya vigogo Simba ya Yanga na pointi tatu nyuma ya wanaoshia nafasi ya tatu, JKT Oljoro, itakuwa na kila sababu ya kuthibitisha ubora wao kama mashabiki wengi wanavyoona.

Usajili mzuri waliofanya wakati wa dirisha dogo kwa kuwaongeza Gaudence Mwaikimba, Kipre Bolou na kiungo Abdi Kasim ni wazi wataweza kulipa kisasi cha kufungwa 1-0 na wapinzani wao hao duru la kwanza.

Wakati huohuo, mchezo wa Ligi Kuu kati ya Toto African na African Lyon uliopangwa kuchezwa Februari 5, na sasa kuchezwa Aprili 18, huku pia mabadiliko hayo yakiathiri mechi za Villa Squad dhidi ya Lyon na Azam na Toto African.

Sababu kubwa ya mabadiliko hayo ni matumizi ya Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ambao tarehe hiyo utatumika kwa sherehe za kichama.

Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema mechi kati ya Villa na Lyon utachezwa Aprili 22 badala ya Aprili 18, huku Azam na Toto wakishuka dimbani Aprili 26 badala ya Aprili 29.

No comments:

Post a Comment