
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga jana walishindwa kukwea kileleni mwa
msimamo wa ligi hiyo baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Moro United katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Yanga ilihitaji ushindi ili kufikisha pointi 30 na kukaa kileleni ikisubiri matokeo ya vinara wa ligi hiyo Simba yenye pointi 28 ambao leo watashuka kwenye uwanja huo kumenyana na Coastal Union.
Matokeo hayo yameifanya Yanga ifikishe pointi 28. Yanga ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza jana kupitia kwa Kenneth Asamoah aliyefunga katika dakika ya 43 baada ya kuunganisha krosi safi ya Haruna Niyonzima kutoka wingi ya kushoto.
Bao hilo liliingia dakika moja baada ya beki wa Yanga, Shadrack Nsajigwa kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kiwiko Benedict Ngassa wa Moro United.
Moro United ilipata bao la kusawazisha katika dakika ya 50 kupitia kwa Ngassa aliyefunga bao hilo kwa kichwa baada ya kuunganisha pasi ya Erick Mawala.
Dakika mbili baadae Davis Mwape aliikosesha Yanga bao baada ya kupiga mpira pembeni huku akiwa peke yake na kipa wa Moro, Jackson Chove.
Baada ya kupata bao la kusawazisha, Moro walibadilika na kulishambulia lango la Yanga
mithili ya nyuki.
Moro ilipata bao la pili katika dakika ya 74 lililofungwa na Simon Suya baada ya kutumia vema makosa yaliyofanywa na beki wa Yanga, Nadir Haroub 'Canavaro'.
Yanga ilisawazisha bao hilo katika dakika ya 79 kupitia kwa Kiiza aliyefunga kwa mkwaju wa penati iliyotolewa na mwamuzi Hashim Abdallah baada ya Salum Kanoni kunawa mpira eneo la hatari.
Katika mechi nyingine iliyochezwa jana, Mtibwa Sugar ilishindwa kuutumia vema uwanja wake wa nyumbani Manungu baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa JKT Oljoro.
Ligi hiyo inaendelea tena leo ambapo mbali na Simba itakayoikaribisha Coastal kwenye Uwanja wa Taifa, Azam itakuwa kwenye uwanja wake Chamazi ikimenyana na African Lyon .
No comments:
Post a Comment