Monday, January 9, 2012
09 JAN. Mancini amlaumu Rooney kwa kadi nyekundu
Roberto Mancini amemshutumu Wayne Rooney kwa kumshinikiza mwamuzi Chris Foy amtoe nje kwa kadi nyekundu Vincent Kompany katika mechi ya Kombe la FA, ambapo Manchester City ililazwa mabao 3-2 na Manchester United siku ya Jumapili.
Mlinzi huyo, kutokana na kadi hiyo atafungiwa kucheza michezo minne baada ya kumchezea rafu Nani kwenye mpambano uliochezwa katika uwanja wa Etihad.
Mancini amesema: "Haikuwa rafu ya kadi nyekundu. Rooney alimuambia mwamuzi nini cha kufanya."
Alipoulizwa kufafanua zaidi iwapo anahisi Rooney alisababisha uamuzi huo utolewe, Mancini ameongeza: "Ndiyo, alikuwa karibu na mwamuzi."
Rooney alijibu kupitia mtandao wa kijamii wa tweeter kwa kuandika: "Inachekesha namna watu wanavyofikiria jinsi Kompany alivyooneshwa kadi nyekundu, mimi si mwamuzi. Sitoi kadi nyekundu. Lakini ilikuwa wazi ni rafu ya kadi nyekundu, kuingia kwa miguu yote miwili."
Mancini amesema klabu yake itakata rufaa juu ya uamuzi huo. Ameongeza: "Tutakata rufaa na nina hakika tutashinda.
"Hakuna sababu yoyote Vincent asicheze mechi dhidi ya Liverpool siku ya Jumatano katika nusu fainali ya Kombe la Carling.
"Ilikuwa ni asilimia 300 haikuwa haki kumtoa kwa kadi nyekundu."
Mlinzi wa Manchester United Rio Ferdinand ametetea kadi hiyo. Aliandika na kuhoji katika tweeter: "Kwa nini kunakuwa na mjadala kuhusu kadi nyekundu? Unapoingia kwa miguu miwili kumkabili mpinzani wako, ni kadi nyekundu. Huo ni ukweli."
Kutolewa kwa Kompany katika dakika ya 12 ilikuwa ni pigo kipindi cha kwanza kwa Manchester City, ambapo Manchester United waliongoza kwa mabao 3-0.
Lakini kikosi cha Mancini kinachoongoza ligi kwa pointi tatu dhidi ya Man United, kilipigana kiume kipindi cha pili na nusura wangesababisha mchezo huo urudiwe, kwani walionekana na nia ya kurejesha mabao yote.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment