Thursday, January 5, 2012
05 JAN. WEMA, DIAMOND KWISHAA!
UCHUMBA wa klabu, usio na radhi ya wazazi kati ya ‘serengeti boy mpenda wakubwa’, Naseeb Abdul ‘Diamond’ na staa wa kitambo Bongo, Wema Sepetu, umevunjwa rasmi.
Mama wa Wema, Mariam Sepetu ndiye aliyeuvunja uchumba huo kwa msisitizo kwamba wakirudiana tena, basi kaburi lake halitakuwa ardhini bali mbinguni.
Mariam amechoshwa na vitendo vya mkwe wa mtaani (Diamond), tabia yake ya kubadili wanawake kama abiria wanavyokalia siti za daladala, imemfanya mama huyo kuapa kiapo kikali.
“Sikufichi mwandishi, kwa kijana yule kurudiana na mwanangu haitawezekana kabisa. Simtaki huyo Diamond, alivyo na tabia yake hafai kuwa na mwanangu.
“Mimi ni mzazi, Wema bado ni mtoto kwangu. Nilijua mapema uchumba wao hautadumu kwa sababu sikuwa radhi kwa hilo.
“Walikutana huko na kuvalishana pete ya uchumba bila kufuata utaratibu,” alisema Mariam.
Mama huyo, akizungumza mbele mwandishi wetu, huku Wema akimsikia, alisisitiza: “Ninachojua ni kuwa mtoto wangu hawezi kurudi tena kwa huyo Diamond.
“Siku ukiona amerudi, ujue maiti yangu itazikwa mbinguni, siyo ardhini.”
Kuhusu hatima ya mwanaye, Mariam alisema kuwa mpaka sasa hajapata mtu aliyemtolea posa, hivyo akaweka wazi kwamba akitokea aliye sahihi, hatasita kumkubali.
“Hajatokea mume hasa wa kumuoa Wema na moyo wangu ukaridhia, wanaokuja ndiyo hao kama huyo Diamond,” alisema.
Amani limebaini kwamba Diamond hana tena nafasi kwa Wema, isipokuwa ‘dogo’ huyo aliyekulia Tandale, Dar, amekuwa akijipendekeza na kujitangaza kuwa bado wapo pamoja.
Katika shoo yake ya kuukaribisha mwaka 2012, iliyofanyika Januari Mosi, ndani ya New Maisha Club, Masaki, Dar, Diamond aliwadanganya mashabiki wake kuwa bado yupo na Wema.
Diamond aliwapiga ‘changa’ mashabiki kuwa Wema ndiye usingizi wake, wakati mrembo aliyedaiwa kuchetuka naye, Jokate Mwegelo, alimtambulisha kwamba ni dada yake.
Mbali na hilo, hivi karibuni, Diamond alimueleza mmoja wa waandishi wa Amani (siyo aliyeandika habari hii) kuwa yeye na Wema bado wapo pamoja.
Alisema: “Hata sasa hivi nimetoka, nimemuacha nyumbani. Tumelala wote.”
Hata hivyo, katika maelezo yake, alikuwa anajikanyagakanyaga kuonesha anachosema kina walakini na mwandishi wetu alipofanya uchunguzi, alibaini kwamba Diamond hakusema kweli.
Diamond na Wema, walianza uhusiano wao mapema mwaka jana.
Oktoba Pili, 2011, Diamond alimvisha pete ya uchumba lakini wakati wa kukaribia kuuaga mwaka, alipigwa kibuti na mrembo huyo, ingawa anajaribu ‘kuuzuga’ ulimwengu kwamba bado wapo pamoja.
SOURCE GLOBAL PUBLISHERS
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment