
Timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes sasa watawakabili Nigeria katika mchezo wa raundi ya pili kusaka tiketi ya kucheza mataifa Afrika machi Mwakani, baada ya kuwaondosha Sudan kwa matokeo ya jumla ya 4-3.
Katika mchezo wa jana usiku uliochezwa katika uwanja wa Khartoum baina ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) na Sudan ulimalizika kwa Sudan kuibuka na ushindi wa goli 2-1, wakati mchezo wa awali uliochezwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam ulishuhudia Tanzania wakíibuka na ushindi wa goli 3-1 na kupelekea matokeo ya jumla kusomeka Tanzania 4-3 Sudan.
Usiku wa jana Sudan walikuwa wa mwanzo kuandika goli katika dakika ya 10 kupitia kwa Mohammed Abdelrahman na dakika mbili mbele Mshambuliaji wa TP Mazembe Thomas Ulimwengu aliisawazishia Ngorongoro Heroes na kupelekea timu kwenda mapumziko zikiwa sare ya goli 1-1.
Vijana wa Sudan waliokuwa wanasaka ushindi wa hudi na uvumba waliandika goli la pili katika dakika ya 65 kwa mkwaju wa penati uliopigwa na Ahmed Nasr na kupelekea mchezo kumalizika kwa Sudan kushinda kwa goli 2-1.
Ngorongoro Heroes iliyofuzu kwa raundi ya pili itaivaa Nigeria julai 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam kabla ya kusafiri kwenda Nigeria kwa ajiri ya marejeano kati ya Agosti 10 na 12 mwaka huu.
Ngorongoro Heroes ambayo inatarajia kurejea nchini jumapili saa 3 asubuhi, ikifanikiwa kuitoa Nigeria, itacheza mechi ya raundi ya tatu na mshindi kati ya Afrika Kusini na Congo Brazzaville. Mechi ya kwanza itakuwa ugenini kati ya Septemba 21 na 23 mwaka huu wakati ya marudiano itakuwa nyumbani Oktoba 6 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment