tuwasiliane

Wednesday, January 18, 2012

18 JAN. Vodacom kuendelea kumwaga fedha TFF


KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania, imemmwagia sifa Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Leodegar Tenga, kwa utendaji wake wa kazi, hali inayowafanya wafikirie kuingia mkataba mwingine wa udhamini wa ligi ya Tanzania Bara.

Mkataba wa Vodacom na TFF unafika tamati Septemba mwaka huu, tangu walipoingia kwa mara ya kwanza, mwaka 2007.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Udhamini wa Vodacom George Rwehumbiza, kampuni yake imetumia zaidi ya Sh bilioni 1.3 kwa ligi nzima, ikiwa ni mpango wenye dira ya kuhakikisha kwamba soka inapiga hatua.

Rwehumbiza alisema mkataba wao mpya watakaoingia mwaka huu, ni matunda ya uongozi bora wa Tenga na timu yake. Alisema wanaamini udhamini wao huo, utaweza kuinua kiwango cha soka. Mzunguko wa pili wa ligi unatarajiwa kuanza Jumamosi.

"Sisi kama Vodacom tutakaa na wenzetu wa TFF kuangalia jinsi tutakavyoongeza udhamini wetu wa ligi ili kukuza zaidi michezo, ingawa tunaamini hayo ni matunda ya Tenga”.

"Mdhamini hawezi kudhamini mahala kama hapana utaratibu mzuri, hivyo haya ni matarajio yetu kuwa tutapiga hatua na kuiweka nchi sehemu nzuri," alisema Rwehumbiza.

Aidha Rwehumbiza alizitaka timu zote zinazotarajia kuingia kwenye ligi hiyo kucheza kwa kujituma ili wajipatie mafanikio ya kuiweka ligi yao katika ushindani wa aina yake.

Kwa sasa Ligi Kuu inashirikisha timu 14 ambazo ni Simba, Yanga, Azam, Mtibwa Sugar, JKT Oljoro, Coastal Union, Villa Squad, African Lyon, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Kagera Sugar, Toto Africans, Moro United na Polisi Dodoma.

No comments:

Post a Comment