
KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic amesema hakuridhishwa na kiwango cha timu yake na hasa katika safu ya ulinzi.
Kutokana na hilo, kocha huyo amesema atalazimika kufanyia marekebisho safu hiyo kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.
Simba ilicheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Tusker ya Kenya juzi na kutoka sare ya bao 1-1.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, kocha Cirkovic alisema, timu yake ilicheza kiwango cha chini tofauti na ilivyocheza kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar.
“Lakini leo (juzi) beki nzima, hasa Juma Nyoso alicheza chini ya kiwango”. Akizungumzia maandalizi ya mechi ya Kombe la Shirikisho, kocha huyo alisema, bado ana muda wa kutosha kuiandaa timu.
Simba inatarajiwa kuanza michuano ya Kombe la Shirikisho ugenini Kigali, Rwanda ambapo itamenyana na Kiyovu ya huko Februari 18.
Naye kocha wa Tusker, Sammy Omollo alisema waliwazidi Simba katika mechi ya juzi hasa kwenye kiungo.
WAKATI HUOHU, PAMBANO la kirafiki la kimataifa kati ya Simba na Sofapaka ya Kenya lililopangwa kufanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam limefutwa na sasa litafanyika jijini Arusha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.Sababu za kupelekewa pambano hilo mjini Arusha ni kutokana na waandajiElite Youth Soccer Academy kudai kupata hasara.
Msemaji wa Elite Youth Soccer Academy, Salum Mkemi alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa taasisi yake imefikia uamuzi huo kutokana hasara waliyopata kwenye mechi kati ya Yanga na Sofapaka Uwanja wa Taifa.
Alisema kuwa hasara hiyo ilisababishwa na mgawo kiduchu Sh3milioni waliopata baada ya mechi hiyo kuingiza Sh16milioni zilizotokana na viingilio.
Alifafanua kuwa taasisi yake ilipata hasara ya kiasi cha Sh14milioni baada ya walitumia Sh18milioni kama gharama maandalizi ya mchezo huo.
"Natangaza rasmi mechi kati ya Simba na Sofapaka iliyokuwa ifanyike leo kwenye Uwanja wa Taifa, sasa haitafanyika tena na badala yake itafanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
"Mabadiliko haya yamekuja kufuatia taasisi yetu kupata hasara kubwa inayofikia kiasi cha Sh 14milioni wakati wa pambano kati ya Yanga na Sofapaka," alisema Mkemi.
Mkemi alilalamikia makato makubwa yanatoyotozwa kwa matumizi ya uwanja huo na kusema yalichangia kwa kiasi kikubwa taasisi yake kuingia harasa.
Juhudi za kuwapata viongozi wa Simba akiwemo msemaji, Katibu Mkuu na Mwenyekiti ili kuthibitisha taarifa hizo hazikufanikiwa kutokana na simu zao kuita bila kupokelewa.Wakati huohuo, Mkemi alisema kabla ya Sofapaka kuvaana na Simba Jumamosi, itatanguliwa na mechi nyingine dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja huohuo.
Aidha, mabingwa watetezi nchini, Yanga wamechomoa kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Tusker ya Kenya kwa madai kwa sasa wanaelekeza nguvu zao kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Moro United kwenye Uwanja wa Taifa.
Tusker ambao juzi walicheza na Simba na kutoka sare ya 1-1 ilikuwa icheze na Yanga jana, lakini Yanga wakadai kuchelewa kupata taarifa za mechi hiyo.Katibu mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa alikiri 'kuipotezea' mechi hiyo kwa kile alichosema ni kuchelewa kufika kwa taarifa.
“Kama washambuliaji wangu wangekuwa makini wangeweza kushinda mechi”.
No comments:
Post a Comment